Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres azindua wito wa kuchukua hatua ili kulinda haki za binadamu duniani

Machafuko katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC yansababisha watu kukimbilia nchi jirani.
UNICEF/Madjiangar
Machafuko katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC yansababisha watu kukimbilia nchi jirani.

Guterres azindua wito wa kuchukua hatua ili kulinda haki za binadamu duniani

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo akiwa Geneva, Uswisi amehutubia Baraza la Haki za binadamu la chombo hicho na kuzindua wito wake wa kuchukua hatua ili kulinda haki za binadamu duniani.

Bwana Guterres amesema kuwa hatua yake hiyo inatokana na ukweli kwamba hata katika miaka 75 ya kuanzishwa Umoja wa Mataifa bado haki za binadamu maeneo mbalimbali duniani zinasiginwa.

Amesema haki za binadamu zinakabiliwa na changamoto kubwa kila uchao, raia wakinaswa kwenye mizozo huku wakiwa na njaa bila kusahau makombora yanayowamiminikia hata wakiwa kwenye maeneo ya raia.

Usafirishaji haramu wa binadamu unaathiri maeneo yote duniani, waathirika wakiwa ni wale walio hatarini na waliokata tamaa. Wanawake na wasichana wanashikiliwa utumwaji, wanakumbwa na ukatili na wananyimwa fursa ya kustawi,”  amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akishiriki kikao cha gazi ya juu cha mkutano wa 43 wa Baraza la Haki za binadamu la UN huko Geneva Uswisi 24 Februari 2020
UN Photo/Violaine Martin
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akishiriki kikao cha gazi ya juu cha mkutano wa 43 wa Baraza la Haki za binadamu la UN huko Geneva Uswisi 24 Februari 2020

Kama hiyo haitoshi amesema kuwa wanaharakati wa mashirika ya kiraia nao wanafungwa jela, vikundi vidogo vya kidini na makabila madogo yanateswa kwa kisingizio cha usalama wa taifa huku waandishi wa habari nao wakiuawa au wakiteswa wakati wanataka kufanya kazi zao.

Ameongeza kuwa vitendo vya chuki navyo ni dhahiri dhidi ya makundi madogo, watu wa jamii ya asili, wahamiaji, wakimbizi na wale waliobadili jinsia za ona wapenzi wa jinsia moja.

“Changamoto mpya nazo zinaibuka kama vile janga la tabianchi, mabadiliko ya makundi ya watu, kasi ya ukuaji wa miji na kasi ya teknolojia. Watu wanaachwa nyuma, hofu inaongezeka, mgawanyiko halikadhalika na baadhi ya viongozi wanatumia shaka na shuku hizo na kufanya hali kuwa mbaya. Mwelekeo wa mahesabu ya kisiasa umeshamiri; gawanya watu ili uongeze kura. Utawala wa sheria umemomonyoka,”  amesema Katibu Mkuu.

Tatiana Mukanire, ni mratibu wa vuguvugu la kitaifa la manusura wa ukatili wa kingono, DRC.
UN News/ Cristina Silveiro
Tatiana Mukanire, ni mratibu wa vuguvugu la kitaifa la manusura wa ukatili wa kingono, DRC.

WITO WA KUCHUKUA HATUA

 Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametaja mambo saba ambayo anaona ni muhimu ili kuweza kurekebisha hali  ya sasa.

 Mosi amesema ni kutambua kuwa haki ni msingi wa maendeleo endelevu kwa kuwa “haki zimetandaa katika ajenda 2030 ya maendeleo endelevu kwa kuwa idadi kubwa ya malengo na malengo madogo yanaendana na haki zinazotambulika kisheria ambazo zimeazimiwa na kila nchi mwanachama.”

Katibu Mkuu amesema kuwa pindi unaposaidia kuondoa watu kwenye umaskini uliokithri, pindi unapohakikisha elimu kwa wote hasa wasichana, pindi unapohakikisha afya kwa wote na kila mtu ana uwezo wa kufanya chaguo lake, “tunawezesha wau kudai haki zao na kuzingatia msingi wa ahadi ya ajenda 2030 ya kutomwacha yeyote nyuma.”

Pili Katibu Mkuu amesema ni haki wakati wa mazingira ya majanga akifafanua kuwa, “haki za binadamu zinakabiliwa na majaribio makubwa pindi mzozo unapoibuka, magaidi wanaposhambulia au janga linapoingia.”

Amesema kuwa sheria za kimataifa za haki za binadamu, sheria za haki za wakimbizi vinaweza kurejesha utu wa kibinadamu katika mazingira yenye giza zaidi.

Amesisitiza kuwa wito huu unatambua kuwa kuheshimu haki za binadamu ni mfumo muhimu wa kuzuia ukiukwaji wa haki. Kwa mantiki hiyo “tutaendelea kushirikisha Baraza la Usalama na vyombo vingine vya Umoja wa Mataifa katika kuongeza uelewa, kuzuia majanga, kulinda wat una kuhakikisha kuna uwajibikaji.”

Wito wa tatu kwa mujibu wa Katibu Mkuu ni usawa wa kijinsia na haki sawa kwa wanawake akisema kuwa, “haki za binadamu katu hazitafanikiwa bila haki za binadamu za wanawake. Na ajabu mwaka huu tukiadhimisha miaka 25 ya hatua za ulingo wa Beijing, bado kuna shinikizo la kurejesha nyuma haki za wanawake. Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana umeshamiri. Sera na sheria zimeundwa kwa kiasi kikubwa kwa kuzingatia uzoefu wa nusu ya wakazi wa dunia.”

Guterres amewaambia washiriki wa mkutano huo wa Baraza la Haki za binadamu kuwa, “tunahitaji kubadili mtazamo wetu wa fikra ili tujenge tukiwa na utambuzi, mifumo ya kijamii na kiuchumi pamoja na kiutawala na ile ya ulinzi ambayo inafanya kazi kwa faida ya wote.”

Katibu Mkuu ametaja wito wa 4 kuwa ni ushiriki wa umma na fursa za haki za kiraia, akisema kuwa wakati huu wa sasa sheria kandamizi zinazidi kusambaa huku uhuru wa kujieleza, dini, ushiriki kwenye mikutano na vikundi ukizidi kubinywa.

“Teknolojia mpya zimesaidia mitandao ya kiraia kupanuka na kukua, lakini pia imepatia mamlaka uwezo wa aina yake wa kudhibiti harakati na kuzuia uhuru,”  amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa hauwezi kufanya kazi yake kwa ufanisi bila ushiriki wa dhati wa mashirika ya kiraia.

Kwa mantiki hiyo amesema wanaimarisha jitihada kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mfumo wa kushirikisha kwa dhati zaidi mashirika ya kiraia ili sauti za mashirika hayo ziweze kupenya katika vyombo vya Umoja wa Mataifa, hususan mashirika ya haki za wanawake na vijana.

Haki za vizazi vijavyo

 Katibu Mkuu ametaja janga la tabianchi kuwa tishio la uhai wa viumbe vya sasa na tayari linatishia haki za binadamu duniani kote na hivyo kutaja haki za vizazi vijavyo kama hatua ya tano.

 Amesema dharura ya sasa ya kimataifa inaangazia jinsi haki za vizazi vijavyo zinapaswa kumulikwa kwa kina zaidi wakati wa kufanyika kwa maamuzi yoyote hivi sasa.

 “Watoto na wajukuu zetu watafurahia haki kidogo sana za msingi iwapo hatutachukua hatua. Tayari tunaweza kuwasikia kupitia sauti jasiri za vijana wa sasa,”  amesema Katibu Mkuu.

Elisabeth Tichy-Fisslberger (kushoto aliyeketi) Rais wa Baraza la Haki za Binadamu akizungumza na Katibu Mkuu wa UN António Guterres kwenye mkutano wa Baraza hilo Geneva Uswisi.
UN Photo/Violaine Martin
Elisabeth Tichy-Fisslberger (kushoto aliyeketi) Rais wa Baraza la Haki za Binadamu akizungumza na Katibu Mkuu wa UN António Guterres kwenye mkutano wa Baraza hilo Geneva Uswisi.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema kupitia mkutano wa tabianchi wa mwezi Septemba mwaka jana, wataweka fursa kwa vijana kwa ajili ya siyo tu kuzungumza bali pia kushiriki na kuandaa maamuzi ambayo yataathiri mustakabali wao.

Hatua za pamoja

Katika hatua hii ya sita Katibu Mkuu anatambua umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa kama msingi wa kushughulikia majanga ya sasa na hivyo kulinda haki za binadamu.

“tutatumia kila fursa kushirikisha wadau mbalimbali, hususan nchi wanachama, kwenye masuala ya haki za binadamu na ubinadamu ikiwemo kuongeza msaada kwa mashirika ya haki za binadamu,”  amesema Katibu Mkuu.

 Mipaka mipya kwa ajili ya haki za binadamu

 Hatua ya saba na ya mwisho ni kuhusu mipaka mipya ya haki za binadamu ambapo Katibu Mkuu amesema zama mpya za digitali zimefungua mipaka mipya ya ustawi wa binadamu, ufahamu na usakaji wa mambo mapya.

 “Lakini bado teknolojia mara nyingi hutumika kukiuka haki za binadamu na faragha kufuatia ufuatiliaji wa maisha ya watu, ukandamizaji na udhalilishaji na chuki mitandaoni,”  amesema Guterres.

 Ameongeza kuwa maendeleo kama vile program tumizi za utambuzi wa sura za binadamu, maroboti na utambulisho wa mtu kidijitali havipaswi kutumika kumomonyoa haki za binadamu, kuongeza ukosefu wa usawa na ubaguzi.

“Jopo huru la ngazi ya juu kuhusu ushirikiano wa kidijitali limeeleza njia ambamo kwayo kila mtu atanufaika kutokana na maendeleo makubwa katika nyanja hii,”  amesema Katibu Mkuu akifafanua kuwa Umoja wa Mataifa utakuwa mchechemuzi wa matumizi ya haki za binadamu mtandaoni na kuwepo na ulinzi wa data hususan zile binafsi na za afya na kwamba ushirikiano na sekta binafsi utakuwa muhimu.