Skip to main content

Bado haki za binadamu zimesalia ndoto kwa wakazi wengi duniani- UN

Watoto wakisoma tamko la haki za binadamu
UN
Watoto wakisoma tamko la haki za binadamu

Bado haki za binadamu zimesalia ndoto kwa wakazi wengi duniani- UN

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema miaka ya 70 ya tamko la haki za binadamu duniani, haijawa tiketi kwa kila mtu kufarahia haki za msingi zilizoainishwa katika nyaraka hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo jijini New York, Marekani kwenye kikao cha ngazi ya juu kuhusu miaka 70 ya nyaraka hiyo na nafasi yake katika kuchagiza malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

“Haki zilizotajwa katika nyaraka hii ya msingi ni haki za kila mtu, popote alipo na hazina mpaka wowote ule iwe ni ule unaoonekana au wa kimaadili. Haki hizi hazibanwi na utaifa, mazingira, jinsia, rangi, dini au imani,” amesema Bwana Guterres huku akinukuu ibara ya kwanza ya tamko hilo inayosema kuwa binadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na sawa kiutu na kihaki.

Hata hivyo amesema cha kusikitisha bado safari ni ndefu ili haki hizo ziweze kufurahiwa na watu wote duniani kote.

“Watu wengi duniani bado wanakumbwa na shida kutokana na haki zao kukiukwa. Ukosefu wa usawa wa kijinsia ni moja ya changamoto kubwa zinazokabili haki za binadamu,” amesema Katibu Mkuu akiongeza pia makundi ya wakimbizi na makabila madogo akisema mara kwa mara wananyimwa haki zao.

Wakimbizi wa ndani kutoka vituo vya kuwalinda raia (PoC site) mjini Juba, wakijificha kutokana na mapigano kati ya SPLA na SPLA-IO.
UN Photo/Eric Kanalstein
Wakimbizi wa ndani kutoka vituo vya kuwalinda raia (PoC site) mjini Juba, wakijificha kutokana na mapigano kati ya SPLA na SPLA-IO.

Bwana Guterres amesema bado kuna upinzani wa kuunga mkono haki za binadamu hususan kwenye nchi ambako haki za binadamu zinaonekana kukiuka masuala ya utaifa.

“Haki za binadamu zinaimarisha serikali na kufanya mamlaka kuwa thabiti zaidi .Tuna Ushahidi wa kutosha ambako ukiukwaji wa haki za binadamu  unaoungwa mkono na serikali ni ishara ya udhaifu na si uthabiti. Mara nyingi ni viashiria vya mzozo na hata kuparaganyika kwa taifa,” amesema Katibu Mkuu.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesihi nchi wanachama kusikia wito huo na kujifunza na hatimaye kusaidia na kuunga mkono hatua za Umoja wa Mataifa za kuimarisha haki za binadamu.

Bwana Guterres amesema “natoa wito kwa nchi ambazo bado hazijatia saini au kuridhia maagano mawili ya haki za binadamu ikiwemo lile la haki za kisiasa na mkataba wa kimataifa wa haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni zifanye hivyo haraka iwezekanavyo.”

Ametumia fursa hiyo pia kukumbusha vijana kuwa wao ndio wahifadhi wa kweli wa tamko la  haki za binadamu hivyo wasonge mbele na kuhoji jinsi ambavyo Umoja wa Mataifa na wanachama wanachukua hatua kwa ajili ya maslahi na haki za binadamu.

Mama mkimbizi  wa Syria aliyekimbia mapigano makali katika mji wa Ghouta anachemsha mayai  akitumia makatarasi magumu kama kuni.
UNHCR/Bassam Diab
Mama mkimbizi wa Syria aliyekimbia mapigano makali katika mji wa Ghouta anachemsha mayai akitumia makatarasi magumu kama kuni.