Hata baada ya kuvuka baharí ya Mediteranea bado maisha ni shubiri kwa wakimbizi-UNHCR

20 Februari 2020

Huko nchini Ugiriki, maisha yamezidi kuwa ya shubiri kwa wakimbizi na wasaka hifadhi waishio kwenye kambi  ya muda ya Moria kisiwani Lesvos, wakati huu ambapo wanaishi watu elfu 10 katika eneo lililokuwa limeandaliwa kuhifadhi watu elfu 3.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR linasema kuwa ugumu wa maisha kwenye kisiwa hicho umezidi hata machungu ambayo wakimbizi na wasaka hifadhi hao walipitia walipovuka bahari ya Mediteranea kusaka maisha bora Ulaya.

Machungu yanayokabili wakimbizi

IOM/Amanda Nero
Wahamiaji wakiwa kando mwa bahari mjini Lesbos, Ugiriki.

 

Wakati huu ambapo Ugiriki imesalia kuwa kituo kikuu cha wahamiaji wanaoingia Ulaya, wakimbizi na wahamiaji wanaofika kambi hii ya Moria wanahaha kuishi kila uchao.

Idadi kubwa ya wakazi wa eneo hili wamekimbia vita, ghasia na ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye nchi zao na wakishaingia wanakabiliwa na kitendo cha kusubiri wiki hadi mwezi kabla maombi yao hayajakubaliwa.

UNHCR inasema wakati wa kipindi cha kusubiri maombi ya ukimbizi au uhifadhi katika nchi nyingine, wakimbizi wanakabiliwa na uhaba wa maji safi na salama, vifaa vya kuwapatia joto, chakula cha kutosha na huduma za afya.

Miongoni mwao ni Sardar, msaka hifadhi kutoka Afghanistan ambaye amesema kuna wakati wanasubiri maji na chakula kwa siku nzima bila mafanikio yoyote huku wagonjwa wakiwa na hali ngumu zaidi, akimzungumzia mkimbizi mmoja akisema kwamba, “hali ni ngumu sana kwa watu hawa. Kama huyu ana saratani lakini hakuna wanachoweza kumsaidia.”

Harakisheni mchakato wa maombi  ya wakimbizi

Ni kwa kuzingatia mazingira duni ya eneo hili, UNHCR inatoa wito kwa serikali ya Ugiriki kuchukua hatua za dharura kushughulikia tatizo la kufurika kwa kambi, kuboresha huduma za kijamii na kuhakikisha inaharakatisha mchakato wa kupitisha maombi ili wakimbizi hao wahamie maeneo ya bara.

Zaidi ya wasaka hifadhi 36,000 hivi sasa wanaishi kwenye vituo vya mapokezi katika visiwa vitano vya Ugiriki ambavyo awali vilipaswa kuhifadhi watu 5,400.

Shirika hilo limesema kuwa suluhu ya kudumu na kuboreshwa kwa mazingira kwenye visiwa hivyo ni muhimu lakini hilo litawezekana pindi idadi ya watu kwenye vituo hivyo vilivyojaa pomoni itakapopungua.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud