Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 80 ya kambi ya wakimbizi huko Lesvos, Ugiriki yateketea, UN yahaha kunusuru

Uharibifu uliosababishwa na moto uliowaka kwenye kituo cha utambuzi wa wakimbizi kwenye kambi ya wakimbizi ya Moria, huko Lesvos nchini Ugiriki.
© UNHCR
Uharibifu uliosababishwa na moto uliowaka kwenye kituo cha utambuzi wa wakimbizi kwenye kambi ya wakimbizi ya Moria, huko Lesvos nchini Ugiriki.

Asilimia 80 ya kambi ya wakimbizi huko Lesvos, Ugiriki yateketea, UN yahaha kunusuru

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashrika ya Umoja wa Mataifa yanahaha kusaidia mamlaka za Ugiriki baada ya moto mkubwa kuteketeza kituo cha mapokezi na utambuzi wa wakimbizi kwenye kambi ya wakimbizi ya Moria usiku wa kuamkia leo Jumatano ya tarehe 9 Septemba.

Miongoni mwa mashirika hayo ni lile la uhamiaji, IOM, ambalo limeeleza kusikitishwa na tukio hilo linaloripotiwa kusababisha wakimbizi na wahamiaji 12,600 kupoteza maeneo ya makazi wakiwemo watoto 400 ambao hawakuw na wazazi wala walezi.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM, António Vitorino, amenukuliwa akisema kuwa janga hilo la kusikitisha linaongeza machungu zaidi kwa watu hao ambao tayari wanakabiliwa na changamoto na mazingira magumu huko Moria ambako kuna mlundikano mkubwa licha ya janga la Corona au COVID-19.

Yaelezwa kuwa asilimia 80 ya kituo hicho imeteketezwa na moto huo na  ambapo Bwana Vitorino amesema, “tunafanya kila tuwezalo kusaidia mamlaka za Ugiriki na wahamiaji na wakimbizi walioathirika ilikuhakikisha wanapata huduma na wanakuwa salama wakati huu ambapo tunahaha kupata suluhu za kudumu.”

Uharibifu uliosababishwa na moto uliowaka kwenye kituo cha utambuzi wa wakimbizi kwenye kambi ya wakimbizi ya Moria, huko Lesvos nchini Ugiriki.
© UNHCR
Uharibifu uliosababishwa na moto uliowaka kwenye kituo cha utambuzi wa wakimbizi kwenye kambi ya wakimbizi ya Moria, huko Lesvos nchini Ugiriki.

Kwa sasa IOM inaangazia zaidi watoto ambao hawana walezi au wazazi ambapo kwa pamoja na wadau wake wameahidi kusafirisha watoto hao 400 kutoka kisiwa cha Lesvos hadi eneo salama la malazi lililoko bara na kuhakikisha kuwa wanakuwa nao hata wakati wa kusubiria kupata huduma.

Shirika hilo limekaribisha hatua ya Kamisheni ya Ulaya ya kufadhili safari muhimu ya watoto hao 400 ikieleza kuwa imejizatiti kusaidia hatua za kupunguza mlundikano kisiwani Lesvos na kuhamishia watoto na familia zao kwenye nchi wanachama wa Muungano wa Ulaya.

IOM pia inapeleka timu ya watendaji wakiwemo wakalimani na wafasiri ili kufanikisha kazi ya kuandaa vituo vya kuhamahama vya kuhifadhi shehena sambamba na kutoa msaada wa malazi kwa wale ambao wamebakia kwenye kituo hicho kilichoungua moto.

Shirika hilo linasaidiana na lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, la kuhudumia watoto, UNICEF, na ofisi ya usaidizi wa kusaka hifadhi ya  Ulaya, na serikali ya Ugiriki katika kuhamishia watu nchi ya tatu.
Mwaka huu pekee, wasaka hifadhi 641 kutoka Ugiriki wamehamishiwa Ubelgiji, Finland, Ujerumani, Ufaransa, Luxembourg na Ureno.

Kituo hicho cha kupokea wasaka hifadhi kilichoko kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa kisiwa hicho cha Lesvos, Mytilene, kwa muda mrefu kimekuwa na mlundikano mkubwa wa wakimbizi na wahamiaji.

Ripoti zinaeleza kuwa, polisi wa kutuliza ghasia walisafirishwa kutoka mji mkuu wa Ugiriki, Athens hadi kisiwani humo ili kuweka vizuizi barabarani kwenye njia zinazotoka na kuelekea kambini Lesovos ili kuepusha wahamiaji waliokuwa wanakimbia kuingia kwenye miji ya jirani, wakati huu ambapo seriklai inaha kusaka makazi ya maelfu yao waliosalia bila makazi.