Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kambi ya Moria kuteketea kwa moto, UNHCR yajenga mahema kunusuru wakimbizi

Watoto wakicheza nje ya kituo cha mapokezi na utambulisho kwenye kambi ya Moria kisiwani Lesvos nchini Ugiriki. Hii ilikuwa mwaka 2018 kabla ya kuungua tena na kuteketea kwa kituo hicho wiki iliyopita.
© UNICEF/Ron Haviv VII Photo
Watoto wakicheza nje ya kituo cha mapokezi na utambulisho kwenye kambi ya Moria kisiwani Lesvos nchini Ugiriki. Hii ilikuwa mwaka 2018 kabla ya kuungua tena na kuteketea kwa kituo hicho wiki iliyopita.

Baada ya kambi ya Moria kuteketea kwa moto, UNHCR yajenga mahema kunusuru wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Hatimaye mamia ya wasaka hifadhi kwenye kambi ya Moria iliyoteketetea kwa moto katika kisiwa cha Lesvos nchini Ugiriki wiki iliyopita, sasa wamepata makazi kwenye mahema yaliyosimikwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.
 

UNHCR inasema kuwa takribani wasaka hifadhi 2,200 wamepatiwa malazi kwenye eneo la dharura ambapo shirika hilo limesimika mahema 280.

Ingawa hivyo, watu wengine 12,000 wakiwemo maelfu ya watoto waliokuwa wanaishi kwenye kambi hiyo, idadi ambayo ni mara nne ya uwezo wake, bado wanalazimika kulala nje au kwenye maegesho ya magari wakisubiri msaada.

Miongoni mwao ni Mostafa Bahadori, aliyezaliwa na kukulia Iran kwa wazazi wa kiafghanistan.

Mostafa na wazazi wake pamoja na mdogo wake wa kiume na dada yake walifika Ugiriki, baada ya kutembea saa 14 kutoka mpaka wa Iran na Uturuki na kisha kufanya majaribio kadhaa ya kuingia kisiwani Lesvos.

 “Unaweza kuona hali yetu’” anasema Mostafa akiongeza, “hatuna  pahala popote, hakuna choo, hakuna maji ya kutosha na hakuna chakula. Leo tumepatiwa mlo mmoja tu na unaona tuko mtaani.”

Nassrulah Paiwandi, mkimbizi kutoka Afghanistan na mwenye umri wa miaka 27, amekuweko kambini Moria kwa mwaka mmoja na nusu sasa na analalala akisema kuwa ana watoto wawili wadogo, hawajala chakula na wana njaa. “Nadhani hatuna mustakabali wowote kwa sababu hali ni mbaya. Hali ni mbayá sana.”

Hatimaye lori lililosheheni mahema liliwasili na UNHCR imefunga mahema ambapo kwa kuanzia ni kwa ajili ya makundi yaliyo hatarini zaidi wakiwemo wanawake, wanaume na watoto.

Mkuu wa ofisi ndogo ya UNHCR huko Lesvos, Astrid Castelein, amesema baada ya matukio matatu ya mioto Moria, kambi nzima imeteketea. Kambi ilikuwa inahifadhi watu 12,000 na wote sasa hawana malazi.

Amesema “hivi sasa tunasafirisha vifaa vya misaada ambavyo ni mahitaji ya msingi na tunasaidia serikali ya Ugiriki kuratibu hatua zinazopaswa kuchukuliwa na kama unavyoona tuko sote hapa kwenye kituo cha muda cha malazi. Yote haya yanafanyika kwa kuzingatia pia kuna janga la gonjwa la Corona, au COVID-19 kwa hiyo tumechukua hatua zote za tahadhari na pia tumeweka vituo vya afya.”