Kinasa sauti nilichopewa na redio ya jamii Karagwe ndicho kimenipa ufaulu wa juu wa masomo:Mhitimu

13 Februari 2020

Mhitimu wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Ruhinda ya Wilayani Karagwe, Kagera nchini Tanzania amekishukuru Kituo cha Redio ya kijamii cha Karagwe kwa kumsaidia wakati wa masomo yake na hivyo kuweza kufaulu mtihani wake wa Taifa kwa kiwango cha daraja la kwanza. 

Ashiru Rwekaza amehitimu elimu ya sekondari kidato cha nne  katika shule ya sekondari Ruhinda ingawa safari yake ya kuisaka elimu hiyo ilighubikwa na viunzi vingi ambavyo kama isingalikuwa redio ya kijamii ya Karagwe asingaliyafikia mafanikio haya.

Ashiru ni kijana mwenye ulemavu wa kutoona pamoja na ulemavu wa viungo vingine na anaishi na mama yake ambaye pia ni mwenye ulemavu, “yaani huyu mzazi wangu asingeweza kumudu kutokana na mahitaji ambayo yalihitijaka shuleni maana na yeye ni mtu mwenye ulemavu, asingeweza kuniwezesha.”

Ashiru alimpoteza baba yake akiwa na umri mdogo na anasema mafanikio katika elimu yake yamesaidiwa kwa kiasi kikubwa na redio Karagwe FM ambayo ni redio ya kijamii ya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera,“msaada ambao nimeupata kutoka redio Karagwe ni msaada mkubwa sana. Kuweza kunisaidia mahitaji ambayo nimekuwa nikiyahitaji mimi, kama mfano ‘tape recorder’ yaani kinasa sauti  ambacho tulikuwa tukikitumia kusomea. Ulikuwa unaichukua hiki kinasa sauti unaanza kumrekodi mwalimu pale anapokuwa darasani. Yote anayoyaongea yanaingia humu kwenye kinasa sauti. Mwalimu akiwa hayupo, unaanza kusikiliza na kuandika au kuhifadhi kichwani.”

Kijana huyu anakishukuru kituo cha redio cha Karagwe ambacho kimempa mafanikio haya,“nimepata ufaulu wa daraja la kwanza ambapo nimeweza kufanya vizuri na kuwa mshindi wa kwanza katika shule yangu. Na siyo mimi niliyefanikisha bali ni uwezeshaji wa redio Karagwe ambao umeweza kunisukuma na kufanya vizuri.”

Mchungaji Godfrey Aligawesa ni Mkurugenzi wa Redio Karagwe anasema,“sisi kama kituo cha redio ambacho kinajali jamii na kinasikiliza matakwa ya jamii na kinasikiliza matakwa ya jamii kadiri ya vipindi vyetu tunavyoendesha, basi tuliwiwa kumsaidia sana kumsaidia Ashiru kutokana na mahitaji yake jinsi alivyoyaleta hapa kituoni.”

Kijana huyo anatamani mafanikio haya yamfikishe katika safari ya kuwa mwanasheria.   

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud