Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la kimataifa la miji lafunga pazia kwa kupitisha azimio kwa ajili ya miji jumuishi na endelevu

Maimunah Mohd Sharif, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Habitat akizungumza katika ufunguzi wa siku ya kwanza ya Kikao cha 10 cha Jukwaa la kimataifa la miji, mjini Abu Dhabi, UAE, 8 Februari 2020
UN-Habitat/Waseem Ali
Maimunah Mohd Sharif, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Habitat akizungumza katika ufunguzi wa siku ya kwanza ya Kikao cha 10 cha Jukwaa la kimataifa la miji, mjini Abu Dhabi, UAE, 8 Februari 2020

Kongamano la kimataifa la miji lafunga pazia kwa kupitisha azimio kwa ajili ya miji jumuishi na endelevu

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa Kumi wa kongamano la kimataifa la miji, WUF10 ambao uliwavutia zaidi ya watu 13,000 walioshiriki katika hafla zaidi ya 540, umefunga pazia kwa wito wa hatua za pamoja kuhakikisha mustakabali bora kwa miji.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la makazi la Umoja wa Mataifa, UN-Habitat, Bi Maimunah Mohd Sharif, amekiambia kikao hicho wakati ya hafla ya kufunga mkutano kwamba  wakati wa mkutano wa siku sita, wajumbe kutoka kila kona ya dunia wamesisitiza juu ya umuhimu wa lengo la pamoja la kuacha urithi wa ulimwengu bora kwa vizazi vijavyo.

Bi. Sharif, amesema, "WUF10 imetupa maoni mazuri juu ya jinsi tunaweza kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Katika WUF10, kupitia vikao 400 vya kuchochea mawazo, maoni kadhaa muhimu yameibuka. "

Kufuatia mkutano huo, washirika wamepitisha azimio la hatua la Abu Dhabi ambayo inajumuisha ahadi kutoka kwa mashirika ya kimataifa, serikali za kitaifa, serikali za mashinani na kikanda, sekta binafsi, asasi za kiraia, wasomi na wengine kwa miaka miwili ijayo na zaidi ya kusaidia kufanikiwa kwa malengo ya maendeleo endelevu.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UN-Habitat amesema Malengo ya Maendeleo Endelevu yanakutanishwa pamoja katika lengo namba 11 la 'miji' la linalolenga kufikia miji jumuishi, salama, inayostahimili na endelevu.

Ameongeza kuwa, “kwa kupitisha azimio hilo la Abu Dhabi, sasa tuna vipengele vya nini, vipi na lini.”

Wazungumzaji wengine katika hafla ya Kufunga mkutano ni pamoja na Katibu Mkuu wa Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD Mukhisa Kituyi, ambaye amezungumza juu ya umuhimu wa kuleta sekta zote pamoja ili kufikiria kuhusu jinsi ya kukabilian na changamoto.

Kwa upande wake   Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, Fabrizio Hochschild Drummond, amesema inatai moyo kuona mchanganyiko wa mtazamo mzuri, tafakari ya vitendo, yatokanayo na mkutano na maoni ya hatua.

Katika ujumbe wa video Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Matiafa, Tiijani Muhammad-Bande, amezungumzia mada ya WUF10 ya Miji ya Fursa: Kuunganisha utamaduni na uvumbuzi akisema "Ni lazima kuchukua hatua za haraka kutumia utamaduni na uvumbuzi kama kichochezi cha kasi ya utekelezaji wa SDGs ikiwa tutatengeneza ulimwengu bora kwa wote. "

Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat ametangaza kwamba Mkutano wa pili wa miji (WUF) mnamo 2022 utafanyika Katowice, Poland - mara ya kwanza WUF imefanyika Mashariki ya Kati Ulaya.