Wakimbizi zaidi wa Cameroon wamekimbilia Nigeria

13 Februari 2020

Takribani wakimbizi 8,000 kutoka Cameroon wamekimbilia katika majimbo ya mashariki na kaskazini mwa Nigeria katika eneo la Taraba na Cross River katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, imeeleza taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Taarifa hiyo ya UNHCR imesema uhamaji huo umefanya jumla ya wakimbizi wa Cameroon nchini Nigeria kukaribia 60,000.

UNHCR imeendelea kueleza kuwa inategemea watu wengine kuingia Nigeria kwani wakimbizi wanaeleza kuwa watu zaidi bado wako katika eneo la mpaka na wanaweza wakawa wako njiani wakitafuta kuingia Nigeria.

Uhamaji huu wa sasa umetokea kabla tu ya uchaguzi mkuu wa Cameroon ambao umefanyika wiki iliyopita ambapo watu walikuwa wakiyakimbia mapigano yanayoendelea kati ya vikosi vya usalama na makundi yanayojihami na silaha. Kuhama huko kunakuja wakati amabpo tayari kuna ongezeko la watu waliofurushwa, hali iliyoshuhudiwa katika robo ya mwisho yam waka 2019 katika maeneo ya Kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa Cameroon.

Wakimbizi wameripoti kuzikimbia vurugu na baadhi yao wameonekana wakivuka mpaka wakiwa na majeraha ya risasi. Kwa mujibu wa wakimbizi wapya, wengi wao wanatoka katika maeneo ya karibu na mpaka wamevuka kupitia nyika na misitu kufika Nigeria.

Jamii wenyeji pamoja na serikali wamekuwa watu wa kwanza kutoa usaidizi ukiwemo wa chakula, malazi na vifaa vya matumizi ya nyumbani ambavyo vinahitajika sana kwa watu hao ambao wameyakimbia makazi yao bila chochote.

UNHCR inakadiria kwamba, “watu wapatao 679,000 tayari ni wakimbizi wa ndani ya Cameroon achilia mbali wale 60,000 ambao wamevuka mpaka kuingia Nigeria.”

Aidha UNHCR imesema inafanya kazi kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha wakimbizi waliofika sasa hivi wanapata malazi angalau katika shule za serikali, katika vituo vya afya au katika familia za wenyeji.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud