Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukuaji wa uchumi duniani bado unasuasua lakini wenye utulivu:IMF

Makonteina katika bandari moja yakionyesha kuimarika kwa uchumi
Photo: Dominic Sansoni/World Bank
Makonteina katika bandari moja yakionyesha kuimarika kwa uchumi

Ukuaji wa uchumi duniani bado unasuasua lakini wenye utulivu:IMF

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti ya shirika la fedha duniani IMF iliyotolewa leo kuhusu hali ya ukuaji wa uchumi duniani katika robo ya kwanza inaonyesha kwamba uchumi wa dunia bado unasuasua ingawa ni wenye utulivu baada ya kushuka kwa miaka miwli mfululizo.

Kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha utafiti cha IM Gita Gopinath kuna matumaini katika ukuaji wa uchumi, "tumeona ishara zenye kuonesha kuwa ukuaji wa uchumi ulimwenguni unaweza kuwa umetulia katika viwango fulani. Tunatarajia ukuaji wa uchumi kutengamaa kwa wastani kutoka asilimia 2.9 mnamo 2019 hadi asilimia 3.3 mwaka huu 2020 na kisha asilimia 3.4 mnamo 2021. "

Ameongeza kuwa kutiwa saini kwa awamu ya kwanza ya mkataba wa biashara baina ya Marekani na Uchina na kufifia kwa hali ya sintofahamu kwa hatua ya Uingereza kujiondoa kwenye Muungano wa Ulaya ni hatua nzuri. Lakini hatari zingine zinajitokeza,"usawa wa hatari iliyopo bado ni mbaya lakini sasa kuna habari njema kutoka kwenye mazungumzo ya biashara baina ya Uchina na Amerika na kutoka kwenye Brexit. Hata hivyo hatari za kijiografia zinaongezeka. Machafuko ya kijamii yameenea katika nchi nyingi na tunaweza kuona kuongezeka kwa mvutano wa kibiashara, "

Kwa kiasi kikubwa kushuka kwa ukuaji wa uchumi India kumechankia katika viwango vya jumla duniani lakini kwa ujumla IMF inaona kwamba uchumi wa dunia unaanza kujerea japo kwa kasi ndogo.

IMF inapendekeza kwamba nchi zenye mzigo mkubwa wa madeni kutafuta uwiano wa gharama zao wakati huu ili ziweze kujiandaa kwa msukosuko wakati ujao. Gopinath amezitaka nchi zilizo na fursa za kifedha kutumia rasilimali hizo kuinua kiwango cha mahitaji kwa kuunga mkono ufufuaji ukuaji wa uchumi kwani ni muhimu pia kwa watunga será kuhakikisha será za fedha zinapaswa kubaki kuwa jumuishi na nchi zinapaswa kuboresha miundombinu ya kijamii, mitaji na miundombinu inayozingatia mabadiliko ya tabianchi.