Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaidhinisha dawa mfanano  ya kutibu saratani ya titi

Ukaguzi wa ziwa na mtu binafsi unashauriwa na madaktari.
National Cancer Institute/Bill Branson
Ukaguzi wa ziwa na mtu binafsi unashauriwa na madaktari.

WHO yaidhinisha dawa mfanano  ya kutibu saratani ya titi

Afya

Hatimaye nuru imeangazia wagonjwa wa saratani ya titi husasan katika nchi za kipato cha chini baada ya shirika la afya duniani WHO hii leo kuidhinisha kutengenezwa kwa dawa ya mfanano ya gharama nafuu iitwayo TRASTUZUMAB. 

WHO inasema kuwa dawa hiyo ya gharama nafuu ni mfano wa ambayo imekuwa ya gharama kubwa na sasa itapatikana kwa wanawake wanaougua saratani kote duniani.

Hii ni mara ya kwanza kwa WHO kuidhinisha uzalishaji kwa gharama nafuu kwa tiba dhidi ya saratani ya titi ugonjwa ambao  unakumba wanawake wengi duniani.

WHO inasema kuwa wanawake milioni 2.1 walipata saratani mwaka 2018 ambapo kati yao hao 630,000 walifariki dunia, na wengi wao ni kwa sababu ya kushindwa kupata matibabu.

Trastuzumab ilijumuishwa katika orodha ya WHO ya dawa muhimu mwaka 2015 kama tiba muhimu kwa takribani asilimia 20 ya saratani ya titi ambapo tayari imeonesha kutibu awamu za mwanzo za ugonjwa wa saratani na wakati mwingine hata hatua za mwisho.

Akizungumzia hatua ya WHO, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesmea ni hatua muhimu sana kuidhinisha TRASTZUMAB kuweza kufikia wanawake wote kokote ulimwenguni.

Amesema wanawake wengi hasa katika nchi maskini wanashindwa kupata matibabu kutokana na gharama kubwa ya dawa.

Gharama halisi ya matibabu ya dawa hiyo kwa mwaka ni wastani wa dola elfu 20 ambapo itakayotengenezwa kufanana nayo itakuwa nafuu kwa asilimia 65.

Tayari uchunguzi umefanyika kuwa inatibu na inaweza kununuliwa hata na mashirika ya Umoja wa Mataifa na hata wazabuni wa kitaifa.

Katika nchi tatu za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, utafiti ulifanyika kwa wanawake 1325 ambapo ilibainika kuwa wanawake 227 hawakuwa wameanza matibabu mwaka mmoja hata baada ya kubainika kuwa na saratani ilihali 185 walikuwa na saratani ya hatua ya 1 hadi ya 3.

Wengi wao walisema hawawezi kusaka tiba kutokana na gharama kubwa ya matibabu.

Mwezi Julai mwaka 2018, WHO  ilizindua mradi wa kifani wa kupanua wigo wa kuidhinisha dawa za matibabu zitokanazo na vyanzo vya kibayolojia au vitu vingine vyenye uhai, au Biotherapeutic kwa lengo la kupunguza gharama za dawa hususan kwa nchi zinazoendelea.

Dawa hizi hutengenezwa kwa kutumia chanjo za matibabu, damu, jeni na tishu pamoja na vitu vingine na kwa hivyo Trastuzumab ni dawa ya kwanza ya mfanano kutokana na mradi huo kifani.