Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko ya matatizo ya afya ya akili miongoni mwa vijana lasukuma UNICEF na WHO kuchukua hatua

Mgonjwa katika hospitali ya magonjwa ya akili mjini Monrovia, Liberia
World Bank/Dominic Chavez
Mgonjwa katika hospitali ya magonjwa ya akili mjini Monrovia, Liberia

Ongezeko ya matatizo ya afya ya akili miongoni mwa vijana lasukuma UNICEF na WHO kuchukua hatua

Afya

Takriban asilimia 20 ya barubaru duniani kote wamekumbwa na magonjwa ya akili na karibu asilimia 15 ya barubaru katika nchi za kipato cha chini na wastani wametafakari kuhusu kujiua, imesema taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la afya ulimwenguni, WHO.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo jijini New York, Marekani, Geneva Uswisi na Florence nchini Italia, wakati kukishuhudiwa viwango vya juu vya kujiumiza, kujiua, wasiwasi miongoni mwa watoto na vijana kote ulimwenguni, UNICEF na WHO wanaungana na wadau katika kutatua changamoto hii inayoendelea kukua.

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amenukuliwa akisema, “watoto wengi na vijana, matajiri na maskini wote katika kona zote za dunia wanakabiliwa na magonjwa ya akili”. Ameongeza kwamba, “janga hilo halina mipaka huku matatizo ya akili yakianza kabla ya umri wa miaka 14, tunahitaji mikakati ya haraka na bunifu katika kuzuia, kuchunugza na iwapo inahitajika kutibu katika umri mdogo”.

Kwa mujibu wa takwimu takriban aslimia 20 ya vijana kote ulimwenguni wanakabiliwa na matatizo ya akili na kujiua ni sababu ya pili kuu ya vifo miongoni mwa vijana wa umri wa kati ya miaka 15- 19 kote ulimwenguni.

Gharama ya afya ya akili haipaswi kuwa jukumu la mtu binafsi, lakini inagharimu jamii na uchumi licha ya kwamba afya ya akili miongoni mwa watoto na barubaru haitiliwi maanani katika program za kimataifa na kitaifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, “ni watoto wachache tu wana uwezo wa kufikia programu zinazowafundisha mbinu za kukabiliana na hisia zao”

Ameongeza kwamba, “ni watoto wachache tu walio na matatizo ya afya ya akili wanfikia huduma wanazohitaji, na hili linahitaji kubadilika”.

Katika lengo la kuchagiza kuhusu afya ya akili, UNICEF na WHO watafanya kongamano la kwanza mjini Florence, Italia kama sehemu ya kongamano la mfululizo wa makongamano ya UNICEF ya Leading Minds ya kuangazia changamoto zinazokabili watoto na vijana katika karne ya 21.