Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi lukuki kusaidia wakimbizi zatangazwa Geneva, Uswisi

Duka la kinyozi katika  kambi ya wakimbizi ya Kakuma, Kenya 2016
Picha/UN-Habitat/Julius Mwelu
Duka la kinyozi katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma, Kenya 2016

Ahadi lukuki kusaidia wakimbizi zatangazwa Geneva, Uswisi

Wahamiaji na Wakimbizi

Mkutano wa kwanza wa ngazi ya juu kuhusu wakimbizi umefunga pazia huko Geneva, Uswisi ukiwa na ahadi lukuki za kusaidia wakimbizi na jamii zinazowahifadhi huku ahadi nyingi zaidi zikijikita katika usaidizi wa muda mrefu hususan  ujumuishaji.

Zaidi ya washiriki 3,000 wakiwa ni wawakilishi wa serikali, mashirika ya fedha ya kimataifa, sekta ya biashara, wahisani wa kibinadamu na maendeleo, wakimbizi na mashirika ya kiraia wameshuhudia zaidi ya ahadi 770 hadi Jumatano mchana.

Ahadi hizo ni pamoja na fursa za ajira, elimu kwa watoto wakimbizi, sera mpya za kiserikali kwa ajili ya wakimbizi, makazi, nishati salama, miundobinu na usaidizi mzuri kwa jamii zinazowahifadhi.

Miongoni mwa makundi yaliyotoa ahadi kubwa zaidi za usaidizi ni serikali, mashirika ya kiraia, vikundi vya wakimbizi, vyama vya michezo na vikundi vya kidini pamoja na sekta binafsi ambapo ubia umeonekana kuwa matokeo  ya mafanikio makubwa zaidi kwa wakimbzi na mara nyingi kwa nchi za kipato cha chini zinazohifadhi wakimbizi.

Jengo hili la maabara ni moja ya majengo matatu yaliyojengwa kwa usaidizi wa serikali ya Japan kwenye makazi ya wakimbizi ya Kyangwali nchini Uganda.
UN News/ John Kibego
Jengo hili la maabara ni moja ya majengo matatu yaliyojengwa kwa usaidizi wa serikali ya Japan kwenye makazi ya wakimbizi ya Kyangwali nchini Uganda.

Huku ahadi zaidi zikitarajiwa siku za usoni, huku vigezo vya kupima mafanikio kama vile kiasi cha ajira kilichotengwa, shule na kupungua kwa kiwango cha umaskini vikiwa vimeshawekwa, Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi amesema “suala la umma kuunga mkono usakaji hifadhi limekumbwa na chuki katika miaka ya hivi karibuni, na katika visa vingi, jamii ambazo zinahifadhi wakimbizi zimehisi kuzidiwa uwezo au kusahauliwa.”

Kwa upande wa fedha, Benki ya Dunia imeahidi zaidi ya dola Bilioni 4.7 kwa ajili ya kusaidia wakimbizi na jamii zinazowahifadhi pamoja na sekta binafsi kwa ajili ya kukuza ajira na kusaidi jamii zinazowahifadhi.

Nayo Benki ya maendeleo ya mataifa ya Amerika iliahidi dola bilioni 1 huku nchi kadhaa na wadau mbalimbali wengine wakiahidi zaidi ya dola bilioni 2 kwa ajili ya ujumuishaji wakimbizi na kusaidia mahitaji ya jamii zinazowahifadhi.

Jukwaa hili ni sehemu ya mkataba mpya wa kimataifa wa wakimbizi uliopitishwa na  nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwezi Desemba mwaka 2018 ambapo mkataba uliweka kanuni kwamba mkutano wa aina hii ufanyike kila baada ya miaka minne ambapo mkutano ujao utafanyika mwaka 2023.

Hata hivyo mkutano wa tathmini ya ahadi zilizotolewa kwenye mkutano huu, utafanyika baada ya miaka miwili.