Ndui ni ugonjwa pekee wa binadamu uliotokomezwa- WHO

13 Disemba 2019

Hii leo kwenye makao makuu ya shirika la afya duniani, WHO huko Geneva, Uswisi kumefanyika tukio maalum la kuadhimisha miaka 40 tangu kutokomezwa kwa ugonjwa wa ndui.

Tukio hilo limefanyika huku ikikumbukwa tarehe 9 mwezi Disemba 1979 ambapo kutokomezwa kwa ndui kulithibishwa na miezi mitano baadaye, mwezi Mei mwaka 1980 mkutano wa Baraza la WHO ulitoa azimio rasmi ya kwamba dunia nzima na wakazi wake sasa hawasumbuliwi tena nan dui.

Ni kwa mantiki hiyo basi katika maadhimisho ya leo, bamba la madini ya shaba liliwekwa katika makao hayo makuu ya WHO kwenye chumba kile kile cha mkutano ambako miongo minne iliyopita wajumbe 19 wa kamishen iyadunia ya kuthibitisha kutokomezwa kwa ndui walikutana na kutangaza kutokomezwa kwa ugonjwa huo.

Akizungumza kwenye tukio hilo lililohudhuriwa na wafanyakazi wa WHO, wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wawakilishi wa nchi wanachama, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema “hii leo ndui ni ugonjwa pekee wa binadamu uliotokomezwa, ushahidi aw ya kile ambacho tunaweza kufanikiwa iwapo  mataifa yatafanya kazi pamoja. Inapokuja magonjwa ya milipuko tuna wajibu wa pamoja na mustakabali wa pamoja. Kwa bamba hili, tunakumbuka mashujaa duniani kote waliokutana na kupigana dhidi ya ndui na kufanya vizazi vijavyo kuwa salama.”

Safari ya kutokomeza ndui

Shirika hilo linasema ndui ulikuwa ugonjwa mbaya sana ambao ulisababisha mateso na vifo katika karne iliyopita ambapo takwimu zinaonyesha watu milioni 300 walikufa nan dui katika karne ya 20 pekee.

Pia ugonjwa huo uliwaacha wengi na matatizo ya ngozi, maumivu makali, ulemavu na theluthi moja ya watu wote waliopata ndui walikufa. Ugonjwa huo ulisambaa kote duniani na kudumu kwa karne. Kisa cha mwisho cha nduo kwa mujibu wa WHO kiliripotiwa Somalia 1977.

Baada ya kuripotiwa kwenye mkutano wa Baraza la afya duniani mwaka 1948 na mwaka 1958 kwenye muungano wa Soviet , Who ilizindua mkakati kabambe wa kutokomeza nduo mwaka 1967. Na leo hii ndui ndio ugonjwa pekee uliowahi kutokomezwa ukiwa ni dhihirisho la wazi wa nini tunaweza kufikia endapo nchi zote zinashirikiana na kufanya kazi pamoja limesema shirika la afya.

WHO inasema mafanikio hayo yakutokomeza ndui yaliipa dunia ari ya kuzindua program za chanjo kwa Watoto na baadaye mkakati wa kutokomeza polio.

Na yale ambayo dunia imejifunza katika kutokomeza ndui yamechangia katika kuimarisha hatua za kufuatilia magonjwa ambazo zimefanikisha katika juhudi za leo za kutokomeza polio.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter