Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19: Sitisha au futa shughuli sasa ulinde uhai badala ya kujuta- WHO

Nchi barani Afrika zinapata chanjo kupitia Kituo cha COVAX.
WHO
Nchi barani Afrika zinapata chanjo kupitia Kituo cha COVAX.

COVID-19: Sitisha au futa shughuli sasa ulinde uhai badala ya kujuta- WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limesihi mamlaka na watu binafsi kuangalia uwezekano wa kufuta au kusitisha kwa muda shughuli za mikusanyiko hivi sasa kama njia mojawapo ya kudhibiti kasi ya kusambaa kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona au COVID-19 hasa wakati huu ambapo aina mpya ya virusi Omnicron inasambaa kwa kasi kubwa kuliko virusi vya awali.
 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus ametoa wito huo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi, akitolea mfano jinsi ambavyo wamelazimika kufuta halfa waliyokuwa wafanye hii leo jijini humo.

Dkt. Tedros amesema “njia ya haraka ya kukabili virusi hivi vipya ni kwa viongozi na watu binafsi kuchukua uamuzi mgumu ambao unapaswa kufanyika ili kujilinda na kulinda wengine. Katika maeneo mengine inamaanisha kufuta au kusitisha matukio kama ambavyo tumefanya leo hapa kufuta hafla ya kukutana.”

Amesema kufutwa au kusitishwa kwa tukio ni jambo bora zaidi kuliko kusitisha uhai wa mtu, “Ni vyema kufuta tukio sasa na kusherehekea baadala ya kusherehekea sasa na kuomboleza baadaye.”

WHO amesema hata waliochanjwa chanjo wanaweza kupata maambukizi ya COVID-19 na hata waliokwishaugua wanaweza kuugua tena kwa hiyo ni vyema kuendeleza hatua za kuepuka mikusanyiko sambamba na kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa sabuni au vitaka mikono.

Amekumbusha kuwa hakuna mtu yeyote anayetaka kukutana tena miezi 12 ijayo na kuanza kuzungumzia jinsi fursa zilipotezwa za kuchukua hatua sahihi na kuwa na mgao sawia wa chanjo au kuzungumzia aina mpya ya virusi vinavyosababisha COVID-19.

“Ili kutokomeza janga hili katika mwaka ujao, lazima tumaliza ukosefu wa uwiano wa mgao wa chanjo, kwa kuhakikisha asilimia 70 ya wakazi wa kila nchi wamepata chanjo ifikapo katikati ya mwaka ujao.

Chanjo ya 9 itaongeza kasi ya upatikanaji wa chanjo

Amekumbusha kuwa hatua ya wiki iliyopita ya WHO kuidhiisha kwa dharura chanjo ya 9 dhidi ya COVID-19 inayotengenenzwa na Taasisi ya Serum nchini India chini ya leseni ya NOVAVA ni moja ya hatua ya kuongeza kasi ya utoaji wa chanjo duniani ili kufikia lengo hilo.

Mwaka huu pekee wa 2021 zaidi ya watu milioni 3.3 duniani kote wamekufa kutokana na COVID-19, ikiwa ni idadi kubwa ikilinganishwa na vifo kutokana na Malaria na UKIMWI.

Kwa sasa kila wiki watu 50,000 duniani kote wanakufa kwa COVID-19 na barani Afrika wimbi la nne la COVID-19 linasambaa kwa kasi chanzo ikiwa ni virusi aina ya Omnicron.

Takwimu za WHO zinaonesha kuwa mwezi uliopita, bara la Afrika lilikuwa na idadi ndogo ya wagonjwa wa Corona lakini wiki iliyopita bara hilo liliripoti idadi kubwa ya wagonjwa wengi katika wiki moja.Ushahidi unaonesha kuwa virusi vya Omnicron vinasambaa kwa kasi kubwa kuliko Delta.