Hatari kubwa yawakabili watoa huduma ya kutapisha vyoo-WHO
Hatari kubwa yawakabili watoa huduma ya kutapisha vyoo-WHO
Hatma ya wafanyakazi katika sekta za usafi na hususani watoa huduma ya kutapisha vyoo kwenye nchi zinazoendelea ni suala linalostahili kushughulikiwa kwa dharura, umesema Umoja wa Mataifa, ukionya kuwa haki zao, afya na hadhi zao ziko hatarini.
Likiangazia hatari inayowakumba mamilioni ya watu wanaosafisha vyoo au watapisha vyoo, mabomba na matenki ya maji taka, kabla ya kaudhimishwa siku ya choo duniani Jumanne Novemba 19, shirika la afya duniani WHO linasema licha ya kuwa watu hao wanafanya kazi muhimu ya umma, afya zao ziko hatarini na wakati mwingi wao hutengwa.
Taarifa ya WHO iliyoambatana na ripoti mpya imesema wafanyakazi hao mara nyingi hukaribiana na uchafu wa kinyesi cha binadamu, na hufanya kazi bila ya vifaa au kinga kwa kutumia mikono yao, suala ambalo huwaweka kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa mengi.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa wanakata tu huduma hiyo muhimu inapofeli, wakati jamii inakumbana na kinyesi cha binadamu kwenye mitaro, mitaani na kwenye mito au wakati vyombo vya habari vinaangazia kifo cha mfanyakazi wa usafi wa kutapisha vyoo ndipo hatma zao zinawekwa wazi.
Juma Ng'ombo ni mfanyakazi wa majitaka kutoka Temeke, jijini Dar es salaam nchini Tanzania.
Mashirika ya kimataifa yakiwemo la Kazi duniani ILO, Benki ya Dunia na lile la Water Aid, yanataja sehemu tisa zilizofanyiwa uchunguzi za wafanyakazi wa usafi kwenye nchi za kipato cha chini na cha wastani wanaotapisha vyoo na matanki ya maji taka na kukarabati mabomba ya maji taka.
Ripoti hiyo inasisitiza kuwa usalama wa usafi lazima uambatane moja kwa moja na mazingira bora kwa wale wanaofanya kazi ya kutunza huduma za usafi na kulinda afya zetu, ikiongeza kuwa wafanyakazi katika sekta ya usafi wamebaguliwa ikilinganishwa na wafanyakazi wa sekta zingine.
Kwa mujibu wa WHO, hali duni za usafi pekee husababisha hadi vifo 432,000 kila mwaka vinavyotokana na kuendesha na pia huchangia kuenea kwa magonjwa mengine .