Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shule za waume na waume wanaotarajiwa kuoa zawa chachu ya amani kwenye familia Burkina Faso

Tangu alipojiunga na shule ya waume, Waimbabie amekuwa akishiriki katika shughuli za nyumbani
World Bank/ Lionel Yaro
Tangu alipojiunga na shule ya waume, Waimbabie amekuwa akishiriki katika shughuli za nyumbani

Shule za waume na waume wanaotarajiwa kuoa zawa chachu ya amani kwenye familia Burkina Faso

Utamaduni na Elimu

Nchini Burkina Faso, aina mpya ya shule zinazofadhiliwa kwa ushirikiano wa shirika la idadi ya watu duniani UNFPA na Benki ya dunia zinabadili tabia ya wanaume waliooa na wanaotarajia kuoa. 

Wakati Waimbabie Gnoumou mwenye umri wa miaka 38, mkulima na baba wa watoto nane alipoanza kuhudhuria shule ya waume na waume watarajiwa, aligundua anaweza kufaanya mambo mengi kuboresha uhusiano wake na wake zake na watoto wake, “nikiri tu kuwa nilikuwa si mtu mwema nyumbani kwangu. Nilipokuwa ninatoka na kunywa pombe na kurejea nyumbani,mara nyingi nilikuwa nagombana na mke wangu na hata nampiga.”

Lakini shule hiyo inaendeshwaje? Bi Marceline Bonde ni mwezeshaji,“tuna fanya shughuli za kuwasaidia wanaume kubadili tabia zao na kuwasaidia wake zao linapokuja suala la huduma za afya.  Vile unavyotakiwa kumsaidia mke wako anapokuwa mjamzito. Ni msaada gani unaweza kutoa wewe kama mume? Tunauliza maswali wanajibu. Wanatuambia kuhusu maisha yao nyumbani. Pia tunaigiza majukumu. Kila mmoja katika kundi anaeleza matatizo yake na kwa pamoja tunapendekeza suluhishisho.”

Je unafahamu shule za kufundisha waume watarajiwa?

Baada ya kuhudhuria mafunzo, amebadilika hata mke wake anammiminia sifa kemkem,“shule ya waume ni kitu kizuri. Awali, kulikuwa na kutokelewana katika nyumba yangu. Hivi sasa hatuna migogoro mingi kama awali. Tangu amehudhuria haya mafunzo, tumerejesha mahaba.”

Naye Gnoumou anaongeza,“mimi na mtoto wangu wa kiume mara nyingi tunaenda kuteka maji ambayo tunayatumia kufua. Njiani tukirudi, tukipata nyama, tunanunua kwa ajili ya nyumbani, wake zangu wanapika, na tunakula wote.”

Bwana Gnoumou anaoenekana ameketi na wake zake wawili na baadhi ya watoto wao wakifurahia maisha.