Skip to main content

Matrilioni ya dola yapotea kwa kutomsomesha mtoto wa kike- ripoti

Wanafunzi wa kike huko El Sereif jimbo la Darfur wakicheza ngoma wakati wa tukio la kitamaduni na michezo shuleni kwao.
UN /Albert González Farran
Wanafunzi wa kike huko El Sereif jimbo la Darfur wakicheza ngoma wakati wa tukio la kitamaduni na michezo shuleni kwao.

Matrilioni ya dola yapotea kwa kutomsomesha mtoto wa kike- ripoti

Utamaduni na Elimu

Nchi nyingi duniani hususan zile za kipato cha chini bado zinaona si mtaji kumpeleka shule mtoto wa kike, jambo ambalo hii leo Benki ya Dunia inasema limepitwa na wakati, kwa kuwa ukiwekeza kwa mtoto wa kike umewekeza kwa dunia nzima.

Fursa finyu za elimu kwa watoto wa kike pamoja na vikwazo vya kumaliza miaka 12 ya elimu husababisha nchi husika kupoteza kati ya a dola trilioni 15 hadi trilioni 30 ambazo zingalichangiwa na watoto hao kupitia nguvu kazi katika jamii zao.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Benki ya Dunia iliyotolewa kuelekea siku ya Malala leo julai 12.

Ikipatiwa jina la Fursa zilizopotezwa- Gharama ya kutompeleka shule mtoto wa Kike, ripoti hiyo inasema hali ni mbaya zaidi kwa nchi za kipato cha chini ambako watoto wa kike wanaohudhuria shule ni chini ya theluthi mbili.

Na hata kwa wale wanaojiunga na shule ya sekondari ya awali ni mmoja tu kati ya watatu ambaye anahitimu masomo hayo.

Nchini Afghanistan, ripoti mpya ya UNICEF inasema watoto wengi hawako shuleni na hii inatokana na vita na imani potofu.
UNICEF/Rezayee
Nchini Afghanistan, ripoti mpya ya UNICEF inasema watoto wengi hawako shuleni na hii inatokana na vita na imani potofu.

Ripoti inasema kuwa elimu ina manufaa makubwa kwa msichana ikiwemo kuwainua kijamii na kiuchumi wao na jamii zao, ikitolea mfano kuwa elimu husaidia kutokomeza ndoa katika umri mdogo na pia kupunguza vifo vya watoto wachanga na utapiamlo.

Akizungumzia ripoti hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Dunia, Kristalina Georgieva amesema katu hawatokubali ukosefu wa usawa wa jinsia ukwamishe maendeleo duniani.

Hivyo amesema wakati umefika kuondoa pengo la jinsia kwenye elimu na kuwapatia wasichana fursa sawa na wavulana ya kufanikiwa kwa maslahi ya kila mtu.

Naye Malala Yousafzai ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel amesema pindi wasichana milioni 130 wanaposhindwa kuwa wahandisi, waandishi wa habari au maafisa watendaji wakuu kwa sababu ya kukosa elimu, dunia inakosa matrilioni ya dola ambazo zingeimarisha uchumi, afya ya umma na utulivu.

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed (kushoto) akizungumza na Malala Yousafzai, mchechemuzi wa haki ya elimu kwa watoto wa kike na pia mshindi mwenye umri mdogo zaidi wa tuzo ya amani  ya Nobel.
UN / Evan Schneider
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed (kushoto) akizungumza na Malala Yousafzai, mchechemuzi wa haki ya elimu kwa watoto wa kike na pia mshindi mwenye umri mdogo zaidi wa tuzo ya amani ya Nobel.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hii leo watoto wa kike milioni 132 wenye umri wa kati ya miaka 6 hadi 17 hawako shuleni na hivyo nchi hususan za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zimetakiwa kuwekeza ili wasichana wapate fursa bora ya kujifunza.