Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufisadi na pengo la usawa vyachochea maandamano duniani- OHCHR

Waandamanaji wakiwa katika mitaa ya La Paz nchini Bolivia.
UN Bolivia/Patricia Cusicanqui
Waandamanaji wakiwa katika mitaa ya La Paz nchini Bolivia.

Ufisadi na pengo la usawa vyachochea maandamano duniani- OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR hii leo imetoa taarifa yake ikipazia sauti mwenendo wa maandamano yanayoendelea maeneo mbalimbali dunia ikisema kuwa ni kiashiria tosha cha wananchi kuchoshwa au kuchukizwa na serikali zao hususan kutokana na hali ngumu za kiuchumi na kijamii, ufisadi, ukosefu wa usawa na kuongezeka kwa pengo la walio nacho na wasio nacho.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa ofisi hiyo, Ravina Shamdasani amesema hisia hizo za wananchi zinachochewa zaidi na kuongezeka kwa ukosefu wa imani kwa taasisi za serikali, wanasiasa na viongozi.

Ametaja maeneo ambako maandamano yanapamba moto kuwa ni Bolivia, Chile, Hong Kong, Ecuador, Misri, Guinea, Haiti, Iraq na Lebanon bila kusahau ambako maandamano yalishika kasi mapema mwaka huu huko Algeria, Honduras, Nicaragua, Malawi, Urusi, Sudan na  Zimbabwe, pamoja na nchi za Muungano wa Ulaya kama vile Ufaransa, Uingereza na Hispania.

Bi. Shamdasani amesema, “baadhi ya maandamano haya yamechochewa na kitu kimoja au viwili na kisha kusambaa na kudhihirisha wananchi kutoridhishwa na hali za kisiasa, kiuchumi na kijamii.”

 Amefafanua kuwa baadhi  ya maandamano yameshika kasi kutokana na “hatua dhaifu zinazochukuliwa na serikali au matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji, hali ambayo imesababisha makumi ya maelfu ya watu kumiminika mitaani kuonyesha mshikamano na wale waliouawa au waliojeruhiwa au waliokamatwa na vikosi vya usalama.”

 Msemaji huyo ameongeza kuwa mara nyingi vikosi vya usalama vimeshindwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya matumizi ya nguvu na kujaribu kuzuia h aki za msingi za kibinadamu kama vile uhuru wa kukusanyika au kuandamana kwa amani na uhuru wa kujieleza.

Baadaye hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres atazungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuhusiana na mwelekeo wa maandamano maeneo mbalimbali duniani.