Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wawili wauawa Mali, UN yalaani vikali

Picha:Unifeed Video
Moja ya majeneza yaliyokuwa yamehifadhi miili ya walinda amani kutoka Chad waliouawa nchini Mali wakihudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSMA(Maktaba).

Walinda amani wawili wauawa Mali, UN yalaani vikali

Amani na Usalama

Walinda amani wawili wa Umoja wa Mataifa kutoka Chad wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa baada ya kushambuliwa wakiwa kambini mwao Kaskazini mwa Mali Alihamisi usiku. Kwa mujibu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSMA shambulio hilo lililotokea eneo la Aguelhoc jimbo la Kidali lilikuwa la mivurumisho ya risasi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio hilo na  kukumbusha kwamba mashambulizi dhidi ya walinda amani yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa. Ameongeza kuwa mashambulio hayo hayaukatishi tamaa Umoja wa Mataifa bali yanauongezea ari na dhamira ya kuwasaidia watu na serikali ya Mali katika nia yao ya kusaka amani ya kudumu.

Nalo baraza la usalama la umoja wa Mataifa likilaani shambulio hilo limeitaka pia serikali ya Mali kuchunguza tukio hilo na kuhakikisha wahusika wanafikishwa mbele ya mkono wa sheria. Limesisitiza kuwa kushiriki kupanga, kusimamia , kufadhili au kuamrisha kufanyika kwa mashambulizi dhidi ya walinda amani wa MINUSMA ni msingi wa kuwekewa vikwazo vikali kwa mujibu wa maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.