Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twahitaji ujasiri zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote kutatua changamoto za dunia- Macron

Emmanuel Macron, Rais wa Ufaransa, akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (24 Septemba 2019)
UN/Cia Pak
Emmanuel Macron, Rais wa Ufaransa, akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (24 Septemba 2019)

Twahitaji ujasiri zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote kutatua changamoto za dunia- Macron

Amani na Usalama

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amehutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo Jumanne jijini New  York, Marekani akitaka mwelekeo wa kijasiri zaidi katika kutatua vitisho vikubwa vinavyokabili dunia hivi sasa.

Akianzia na Iran, Rais Macron amesema, “ongezeko la mvuatno tangu tarehe 14 mwezi Septemba baadaya mashambulio dhidi ya Saudi Arabia, yameongeza hatari zaidi ya mzozo unaoweza kuibuka kwa uchukuaji hatua usio na kipimo.”

Amesema, “hivi sasa kuliko wakati wowote ule, ninaamini kwa dhati kuwa wakati umefika wa kurejelea mashauriano baina ya Marekani, Iran na watiaji saini wa mkataba wa pamoja wa programu ya nyuklia ya Iran, JCPOA na mataifa ya kwenye ukanda huo ambayo ndiyo ya  kwanza yatakayoathirika na ukosefu wa utulivu na usalama utokanao na mvutano huo.”

Amegusia pia suala la mabadiliko ya tabianchi akiasema tabianchi ni moja ya mafanikio ya ushirikiano thabiti wa sasa wa kimataifa.

Rais huyo wa Ufaransa amefafanua kuwa, “tulionesha uthabiti huo baada ya Marekani kujitoa kwenye mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi. Kwa pamoja Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia, tulikuwa na mkutano wa ngazi ya juu wa Sayari. Tumewezesha kushirikisha wadau wengine pamoja na kupata fedha kutoka maeneo mengine. Tulishuhudia jana kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa hatua kwa tabianchi.”

Kuhusu suala la kutoweka kwa kuaminiana jambo ambapo hata Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Profesa Tijjani Muhammad-Bande amekuwa analisisitiza, Rais Macron amesema, “kujenga amani ni kuweka hali yako rehani; kuamua kushiriki kwenye mazungumzo, kulegeza misimamo, kujenga upya imani. Na katika maeneo mengi, hilo ndilo jambo tunahitaji.”