AU na FAO kuimarisha uchumi wa kilimo ili kumkomboa mwanamke Afrika

28 Novemba 2019

Muungano wa Afrika AU na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO wamesema wanaimarisha ushirikiano wao ili kuhakikisha uchumi wa kilimo barani Afrika unaleta tija kwa mamilioni ya watu wa bara hilo.

Hayo yamejitokeza katika mazungumzo baina ya mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu na kamisha wa masuala ya uchumi na kilimo wa AU Bi Yosefa Leonel Correia Saccko mjini Roma Italia.

Wawili hao wamejadili masuala mbalimbali ya kuimarisha na kuendeleza kilimo barani Afrika katika nyakati hizi za mabadiliko ya tabianchi, kuboresha ushirikiano wao na kubwa zaidi kuimarisha masuala ya takwimu kama anavyofafanua Bi Sacko "Tunataka kuimarisha ushirika na FAO hasa katika ukusanyaji takwimu tunataka kuimarisha kwa sababu tunachangamoto kubwa katika upande wa takwimu za kuaminika. Na hi indio sababu nimeongea na mkurugenzi  na amekubali kwamba tuendelee na kulitilia mkazo.”

Amesewma suala lingine watakalolitilia mkazo ni kumkomboa mwanamke mkulima wa Afrika kutokana na kilimo cha jembe la mkono

“Unajua kwamba asilimia 62 ya wafanyakazi katika sekta ya kilimo ni wanawake, na tumezindua kampeni ya kwamba ya mitambo ili kuliweka jembe la asili la mkono kwenye makavazi na kukifanya kilimo kuwa cha kisasa ili kuondoa shulba zote hizo ambazo wanawake wamekuwa wakikabiliwa nazo katika zama hizo, tunataka kuleta teknolojia, masuala ya kidijitali, ubunifu kwa wanawake ili waongeze uzalishaji.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud