Marufuku ya biashara ya meno ya tembo wa Afrika yaendelea

28 Agosti 2019

Mkutano wa 18 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa kusimamia viumbe pori vilivyo hatarini kutoweka CITES umemalizika huko Geneva, Uswisi kwa kuimarisha hatua za kudhibiti biashara ya wanyamapori na mimea pori.
 

Lengo ni kuhakikisha matumizi endelevu ya viumbe hivyo ambapo nchi wanachama wa mkutano huo, CoP18 waliangazia mapendekezo ya kutaka kulegeza au kukaza masharti ya biashara ya viumbe hivyo ikiwemo tembo wa Afrika, Kakakuona, vifaru, aina za miti ya kipekee na hata maua ambayo hutumika kwenye dawa.

Kwa kukaza masharti, viumbe vinaowekwa katika orodha ya kwanza ili kuhakikisha biashara yake inadhibitiwa kwa kiwango cha juu kwa kuwa viko hatarini kutoweka.

Orodha ya pili ni kwa viumbe ambavyo si lazima viko hatarini kutoweka lakini biashara yake ni lazima isimamiwe vizuri ili uwepo wao uwe endelevu ilhali orodha ya tatu ni kwa viumbe ambavyo angalau vinapatikana kwenye nchi moja na nchi hiyo imeomba usaidizi wa CITES katika kudhibiti.

Mathalani kwa upande wa twiga ambao mkutano umebaini kuwa idadi yao imepungua kwa kati ya asilimia 36 hadi 40 katika kipindi cha miongo mitatu iiliyopita, wajumbe wameamua kumuweka kwenye orodha ya II.

Uamuzi kuhusu tembo

UNEP GRID Arendal/Peter Prokosch
Kati ya mwaka 2010 na 2012, tembo 100,000 waliuawa barani Afrika kwa ajili ya meno yao.

Wajumbe pia walitathmini hatua za kuuza nje ya nchi tembo walio hai kuelekea maeneo sahihi na yanayokubalika ambapo mauzo hayo yatakubalika katika mazingira mahsusi baada ya mashauriano na CITES na vyombo vya kimataifa vya uhifadhi ikiwemo IUCN na iwapo usafirishaji huo utakuwa na manufaa ya  uhifadhi.

Kuhusu pendekezo la meno ya tembo wa Afrika, mkutano umekataa ikimaanisha ya kwamba marufuku ya biashara hiyo inaendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa CITES, Ivonne Higuero amesema, “binadamu anapaswa kuchukua hatua dhidi ya kutoweka kwa viumbe kwa kubadili mbinu za usimamizi wa wanyamapori na mimea pori duniani. CITES inatunza mazingira yetu kwa kuhakikisha kuwa biashara ya kimataifa ya mimea na wanyamapori inafanyika kisheria, ni endelevu na inafuatiliwa. Biashara inayosimamiwa vizuri ina mchango mkubwa kwa ustawi wa binadamu, kujipatia kipato chake na mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu, SDG.”

Wajumbe walikubali hata hivyo ombi la Afrika Kusini la kuengua biashara ya mmea wa Aloe ambao ni maarufu katika utengenezaji wa dawa kutoka kwenye mifumo ya kupatia kibali na kwamba athari zozote za uamuzi wa sasa zitafuatiliwa kwa karibu.

Mkutano wa 18 wa nchi wanachama wa CITES utafanyika Costa Rica m waka 2022.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud