Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujangili waendelea kutishia mustakabali wa tembo Afrika:CITES

Tembo na ndege katika makazi yao ya asili huko Ghana
World Bank/Arne Hoel
Tembo na ndege katika makazi yao ya asili huko Ghana

Ujangili waendelea kutishia mustakabali wa tembo Afrika:CITES

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Tathimini mpya iliyofanywa na ofisi ya mkataba wa kimataifa kuhusu biashara ya viumbe vilivyo hatarini CITES katika kitengo chake cha uafuatiliaji wa mauaji haramu ya tembo (MIKE) umethibitisha kwamba ujangiri unaendelea kuwa tishio kubwa kwa mustakabali wa tembo barani Afrika.

Kitengo hicho cha MIKE kimetoa tathimini hii kwa kuangalia idadi na kiwango cha mauaji haramu ya tembo na kugawanya na idadi ya mizoga ya tembo inayokutwa na askari wa Wanyama pori wakiwa katika doria barani Afrika.

Kwa mujibu wa tathimini hiyo endapo “kiwango nicha juu  zaidi ya 0.5 inamaanisha kwamba mauaji zaidi ya tembo yaliyoripotiwa yametokana na ujangiri kuliko sababu zingine au vifo vya kawaida. Na ushahidi uliokusanywa unaonyesha kwamba kiwango cha mauaji haramu ya tembo kiliongezeka mwaka 2011 na kufikia 0.77, wakati ambapo ujangiri dhidi ya tembo wa Afrika ulikuwa asilimia 10. Kufikia mwaka 2017 kiwango kilishuka kidogo hadi 0.53 na kimesalia hapo hadi mwaka jana.”

CITES imesisitiza kwamba kiwango kikubwa cha mauaji haramu ya tembo kinatia hofu “kwa sababu  hata katika maeneo ambayo yaweka ulinzi mzuri wa idadi ya tembo wao  vifo vya tembo vitokanavyo na ujangiri haviwezi kufidiwa na idadi ya tembo wanaozaliwa.”

Hali halisi

Barani Afrika idadi ya tembo ni ndogo , wametawanyika na hawana ulinzi mzuri kwa mujibu wa tathimini na hivyo kuwafanya tembo katika bara hilo kuwa katika hatari kubwa dhidi ya vitendo vya ujangiri.

Wakati kiwango cha mauaji ya tembo kikisalia katika 0.5, idadi ya tembo kutoka Afrika walio katika nchi zingine inaendelea kupungua .

Tathimini hiyo mpya ya CITES imesema ripoti ya hali ya tembo barani Afrika iliyotolewa mwaka 2016  inakadiria kwamba idadi ya tembo barani humo imepungua sana kutoka milioni 12 karne iliyopita hadi kufikia 400,000 hivi sasa.

Na imetoa wito kwa nchi, asasi za kiraia na wadau wengine wote wanaohusika na masuala ya Wanyama pori kuchukua hatua Madhubuti ili kuhakikisha tembo hao wanalindwa la sivyo wako katika hatari kubwa ya kutoweka.