Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia wa UN na mashirika ya kiraia ni muarobaini wa kufanikisha SDGs- Espinosa

Washiriki katka mkutano wa 68 wa UN na mashirika ya kiraia huko Salt Lake City jimboni Utah, nchini Marekani. (28 Agosti 2019)
UN News/Conor Lennon
Washiriki katka mkutano wa 68 wa UN na mashirika ya kiraia huko Salt Lake City jimboni Utah, nchini Marekani. (28 Agosti 2019)

Ubia wa UN na mashirika ya kiraia ni muarobaini wa kufanikisha SDGs- Espinosa

Masuala ya UM

Ubia kati ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia na vijana ni muhimu katika kufanikisha makubaliano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Hiyo ni kauli ya Marie Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa aliyotoa huko Salt Lake City jimboni Utah, nchini Marekani mwishoni mwa mkutano wa UN na mashirika ya kiraia.

Mkutano huo wa siku tatu uliomalizika leo jumatano ulilenga kuona ni kwa vipi Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia wanaweza kusongesha ajenda 2030 ya maendeleo endelevu ambapo Bi. Espinosa amesema, “licha ya maendeleo yaliyopatikana kwa binadamu tangu kuanzishwa mwa Umoja wa Mataifa miaka 74 iliyopita, bado idadi yao kubwa wanakabiliwa na machungu.

Ametaja ukosefu wa usawa, ukosefu wa usalama na ongezeko la madhara ya utawandawazi mambo ambayo yamechochea kushamiri kwa chuki dhidi ya uhusiano wa kimataifa, ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na vita.

 “Kila uchambuzi unaonesha kuwa changamoto hizi hazitaweza kushughulikiwa iwapo hatutafanya kazi pamoja. Kadri dunia yetu inavyozidi kuingiliana, shida inayoingia taifa moja, inagusa taifa lingine na mbinu za kujipatia kipato vivyo hivyo kwa hiyo ni dhahiri kuwa tunahitaji kushirikiana zaidi na si kutengana,” amesema Bi. Espinosa.

Amepongeza mchango wa mashirika ya kiraia katika kuunda kazi za Umoja wa Mataifa kuanzia mwanzo wa chombo hicho kwenye kutambua haki za wanawake na wanaume, haki za mtoto, haki za watu wa jamii ya asili, na haki za watu wenye ulemavu.

 “Nawasihi muendelee kushirikiana na serikali zenu kuhakikisha kuwa mnatumia fursa hizi ili kutuweka sawa na shirikianeni na jamii zenu kusaka suluhu za shida kule mashinani na suluhu hizo zinaweza kuigwa kwingineko,” amesisitiza Rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

María Fernanda Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akihutubia wajumbe wa mkutano wa 68 wa UN na mashirika ya kiraia huko Salt Lake City, Utah nchini Marekani, (28 Agosti 2019)
UN News/Conor Lennon
María Fernanda Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akihutubia wajumbe wa mkutano wa 68 wa UN na mashirika ya kiraia huko Salt Lake City, Utah nchini Marekani, (28 Agosti 2019)

Nyaraka ya mwisho iliyotokana na mkutano huo, inaonesha msisitizo wa wanarahakati katika umuhimu wa kutambua miji na jamii kama msingi wa mafanikio ya SDGs na kusisitiza umuhimu wa ujumuishi, amani, familia, elimu, vijana na uwezeshaji wa wanawake na wasichana.

Ijapokuwa msisitizo wa mwaka huu wa mkutano huo ulikuwa Miji jumuishi na jamii, nyaraka hiyo ya mwisho imetambua muingiliano kati ya ustawi wa maeneo ya mijini na vijijini pamoja na umuhimu wa kushughulikia mahitaji ya kipekee ya mazingira ya milimani na mataifa ya visiwa vidogo.

Vijana na hatua dhidi ya tabianchi

Umuhimu na uwezo wa vijana ulitambuliwa pia katika nyaraka hiyo ya mwisho ya mkutano ya kwamba vijana walikuwa na nafasi kubwa katika mkutano huo wa mwaka huu.

Uanaharakati na uchechemuzi wa vikundi vya vijana wakati wa mkutano huo ulikuwa dhahiri ambapo katika nyaraka ya kando, kulipitishwa nyaraka ya vijana ya tabianchi ya Salt Lake City.

Nyaraka hiyo inajumuisha vipengele vya utekelezaji kuanzia kutunga sera dhidi ya vitendo vinavyoharibu mazingira, kuelimisha jamii kuhusu faida za mbinu bora za maisha zisizoharibu mazingira, njia nzuri za usafii hadi michezo mizuri kwa mazingira kama vile kutembea na kuendesha baiskeli.

Nyaraka hiyo ilitangaza kuwa, wakati dunia inaelekea katika kiwango cha juu zaidi cha kushuhudia uharibifu, vijana ni wakati wao wa kuungana na kuchukua hatua dhidi ya janga la tabianachi, na kuunganisha nguvu zao ili kujenga dunia isiyo na janga la tabianchi.