Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa CITES waanza leo, kakakuona miongoni mwa wanyama wa kudhibitiwa zaidi

CITES CoP18
CITES
CITES CoP18

Mkutano wa CITES waanza leo, kakakuona miongoni mwa wanyama wa kudhibitiwa zaidi

Masuala ya UM

Wawakilishi wa nchi 183 wanachama wa mkataba wa kimataifa wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka, CITES wanaanza mkutano wao wa siku 11 hii leo huko Geneva, Uswisi kwa lengo la kuimarisha mikakati ya kulinda viumbe hao.
 

Katibu Mkuu wa CITES Ivonne Higuero amesema kuwa tayari nchi hizo wanachama zimewasilisha mapendekezo 56 yenye lengo la kubadili na hatimaye kuimarisha kanuni za kulinda viumbe vya porini wakiwemo wanyama pamoja na maua, ambavyo vinauzwa kwenye soko la kimataifa.

“Mapendekezo mengi yanalenga kuhakikisha kuwa viumbe hivyo vilivyoko hatarini na ambavyo vinaendelea kuuzwa, vinasalia endelevu na hivyo mapendekezo yanataka vibali kutoka CITES ili kuruhusu biashara yao,” amesema Higuero.

Ivonne Higuero, Katibu Mkuu wa CITES
Massimo Gianelli
Ivonne Higuero, Katibu Mkuu wa CITES

Amesema mapendekezo mengine yanataka kupigwa marufuku kwa biashara za viumbe vilivyoko kwenye orodha I ilihali mengine yanataka kuwa viumbe ambavyo tayari idadi yao imekaa sawa vihamishwe kutoka orodha ya I kwenda orodha ya II ya mkataba wa CITES.

 “CITES inaweka kanuni za biashara ya kimataifa kwa mimea na wanyama. Ni mbinu nzuri ambayo inalenga kuhakikisha uwepo endelevu wa viumbe hivyo na kukabiliana na upotevu wa bayonuai,” amesema Katibu Mkuu huyo wa CITES.

Amekumbusha kuwa kanuni zilizo wazi na zinazotekelezeka kwa kuzingatia sera thabiti ni muhimu katika kulinda utajiri wa asili na kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ambayo yalipitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2015.

Ripoti ya mwezi Mei mwaka huu kuhusu bayonuai ilithibitisha kuwa baadhi ya viumbe na mimea iko hatarini kutoweka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matumizi kupita kiasi , uwindaji haramu na uvuvi haramu na ukataji magogo.

Ni kwa mantiki hiyo mkutano huu wa 18 wa CITES utaangazia wanyama, ndege, nyoka, miti na mimea mingine.

Orodha 20 za viumbe hivyo inatokana na hofu juu ya ongezeko la biashara ya wanyama wafugwao, halikadhalika samaki wa hali ya juu na miti pamoja na tembo wa Afrika.

Wajumbe pia wataamua iwapo ala za muziki zitengenwazo kwa miti ya thamani zitolewe kwenye udhibiti kwa mujibu wa CITES.

Mkutano wa CITES unafanyika Geneva, Uswisi na miongoni mwa wanyama wanaomulikwa ni tembo.
World Bank/Flore de Preneuf
Mkutano wa CITES unafanyika Geneva, Uswisi na miongoni mwa wanyama wanaomulikwa ni tembo.

Wanyama na mimea iliyo hatarini na inayopendekezwa udhibiti zaidi

Miongoni mwa wanyama wanaopendekezwa kuwa wahamishiwe kutoka orodha ya II hadi ya I ili udhibiti uwe wa juu zaidi ni kakakuona ambaye magamba yake yenye kemikali ya Keratini hutumika kutengeneza dawa za kienyeji za kichina.

Mwingine ni Markhor, ambaye ni aina ya mbuzi wa kienyeji kutoka eneo la Asia ya Kati ambapo Tajikistan inataka mnyama huyu ahamishwe kutoka orodha ya I iliyowekwa mwaka 1975 na kuwekwa orodha ya II kwa kuwa idadi yao imeongezeka.

Afrika Kusini inapendekeza mmea aina ya Bitter Aloe unaotumika kwenye dawa na ambao sasa uko kwenye orodha ya II, usiguswe na CITES kwa maelezo kuwa mbegu yake inasaidia kukuza vipato.

Nayo Kenya, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Mali, Niger na Senegal zinapendekeza twiga ajumuishwe kwenye orodha ya II kwa kuwa idadi yao inapungua.