Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iran waachie huru wanawake waliofungwa kwa kupinga uvaaji wa hijab

Bendera ya Iran (Kati) ikipepea kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani
UN /Loey Felipe
Bendera ya Iran (Kati) ikipepea kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani

Iran waachie huru wanawake waliofungwa kwa kupinga uvaaji wa hijab

Haki za binadamu

Wataalamu 6 wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamelaani hukumu ya muda mrefu wa kifungo jela dhidi ya wanawake watatu nchini Iran ambao wamekuwa wanashikiliwa kiholela kwa kupinga hadharani uvaaji wa hijabu.

Wanawake hao watatu ni Mojgan Keshavarz aliyehukumiwa kifungo cha miaka 23 na miezi 6 jela, huku Yasaman Aryani na Monireh Arabshahi wakihukumiwa kila mmoja kifungo cha miaka 16 jela.

Watatu hao wote walipatikana na makosa ya kukusanyika na kufanya vitendo vya kutishia usalama wa taifa na kufanya propaganda dhidi ya serikali kwa kuhamasisha na kuchochea mmononyoko wa maadili na ukahaba ilhali Bi. Keshavarz alipatikana pia na kosa la kutusi utakatifu.

Kupitia taarifa yao waliyoitoa hii leo mjini Geneva, Uswisi, wataalamu hao wamesema wanatiwa hofu kubwa kwa kuwa kitendo cha kushikiliwa kwa muda mrefu sambamba  na hukumu dhidi yao vinahusiana na haki yao ya msingi ya kujieleza na kukusanyika katika kusaka usawa wa kijinsia nchini Iran.”

Wataalamu hao Wataalamu hao ni Javaid Rehman, Dubravka Šimonović  Michel Forst, Meskerem Geset Techane,  David Kaye na  Ahmed Shaheed  wamesema,“tunasihi mamlaka za Iran zitupilie mbali mashtaka ya aina hiyo na ziwaachie mara moja watetezi wote wa haki za binadamu ambao wamekuwa wanashikiliwa kiholela kwa utetezi wao wa haki za wanawake,” wamesema wataalamu hao.

Wamekubusha kuwa kuheshimu na kusaidia harakati za watetezi wa haki za wanawake ni muhimu kwa ajili ya kufurahia haki za binadamu.

Wataalamu hao wamesema kuwa mashtaka dhidi ya wanawake hao watatu yaliwasilishwa mahakama baada ya video iliyochapishwa mtandao kuwaonyesha wakiwa wanasambaza maua kwenye treni mjini Tehran tarehe 8 mwezi Machi mwaka huu, ambayo ni siku ya wanawake duniani.

Wanawake hao ambao wenyewe hawakuwa wamevaa hijab, walikuwa wanapinga sheria ya Iran inayolazimisha wanawake kuvaa vazi hilo wakitaka kuwepo kwa haki ya mwanamke ya kuchagua kuvaa au kutovaa.

Wataalamu hao wa haki za binadamu, wamekumbusha mamlaka za Iran kuwa, “watetezi wa haki za wanawake ambao wanapinga uwepo wa sheria hiyo ya mavazi wanafanya kazi yao ya kutetea haki za binadamu zinazotambulika duniani kote. Matumizi ya sheria kandamizi ili kuharamisha utekelezaji wa haki yao ya kujieleza na kukusanyika haviendani na wajibu wa Iran kwa mujibu wa sheria za kibinadamu.”