Asante UNHCR kwa kunipa fursa ya kipekee maishani: Mkimbizi Saber 

Piazza Del Duomo nchini Italia.
© UNICEF/Francesco Spighi / The Florentine
Piazza Del Duomo nchini Italia.

Asante UNHCR kwa kunipa fursa ya kipekee maishani: Mkimbizi Saber 

Wahamiaji na Wakimbizi

Programu ya kimataifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwa ushirikiano na serikali ya Italia ya kuwasaidia wakimbizi kupata elimu ya juu nchini Italia imekuwa ni ngazi ya kufikia matarajio ya mkimbizi Saber ambaye kwa miaka 19 alikuwa akiishi kwenye kambi ya wakimbizi nchini Ethiopia.

Saber mkimbizi kutoka Sudan Kusini ambaye sasa ana umri wa miaka 22 anasema  kwake bado ni kama ndoto kuweza kufika Italia na kuanza kusoma chuo kikuu, ni fursa ya kipekee maishani. 

Safari yake ilianzia kambini Ethiopia baada ya yeye na wazazi wake kukimbia vita Sudan miaka 19 iliyopita akiwa na umri wa miaka 2 na kwa miaka 19 ameishi kwenye kambi ya wakimbizi Ethiopia akiwa na ndoto za kupata elimu ya juu huku akilazimika kutembea kilometa 16 kila siku kwenda shuleni. 

Lakini sasa ndoto zake zimetimia anasomea masuala ya maendeleo ya kimataifa katika chuo kikuu cha Milan, asante kwa program ya UNHCR na serikali ya Italia ya kuwapa ufadhili wa kusoma wakimbizi. 

Anasema ni kozi nzuri inamfunza mengi ikiwepo suala la haki za binadamu ambalo hakujua chochote hapo kabla na sasa analielewa vilivyo. 

Kwa mujibu wa UNHCR hii ni fursa ya kipekee kwani duniani kote ni asilimia 3% tu ya wakimbizi ndio wanaobahatika kufika chou kikuu. 

Saber anasema kukulia kambini si jambo rahisi n ani suala ambalo mtu halitegemei na anakabiliwa na matatizo ya kisaikolojia, kupoteza ndugu na jamaa wa familia n ahata kule anakokuita nyumbani na kila kitu hata huduma za msingi kama elimu, chakula, malazi na mavazi ni hali ngumu. 

Lakini sasa akiwa na umri wa miaka 22 na fursa aliyonayo ana mipango mikubwa ya kumaliza masomo na kurejea kuisaidia jamii yake ili watoto wengi zaidi wapate fursa ya elimu ya juu kama aliyoipata yeye kwani mara nyingi ni finyu sana kwa wakimbizi.