Idadi ya wahamiaji waingiao Ulaya kupitia Mediteranea yapungua- IOM

22 Juni 2018

Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa-IOM linasema idadi ya wahamiaji na wakimbizi waliovuka bahari ya Mediteranea mwaka huu wa 2018 sambamba na wale waliokufa maji imepungua ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Takwimu zinaonyesha kuanzia mwezi Januari hadi sasa  wahamiaji na wakimbizi 40,944 ndio waliingia bara la Ulaya kwa njia ya baharí ilhali mwaka jana katika kipindi hicho ilikuwa 84,675 .

IOM inasema kuhusu idadi ya vifo, kuanzia mwaka huu hadi tarehe 21 mwezi huu ni watu 960 tu waliopoteza maisha baharini ilihali katika kipindi kama hicho mwaka jana ni vifo  2,133.

Flavio Di Giacomo, kutoka IOM ofisi ya Roma, Italia amesema kwa ujumla kiwango hicho cha mwaka huu kikilinganishwa na mwaka jana ni pungufu kwa asilimia 25.

Ikichambua takwimu zake kwa kila nchi ili kudhihirisha kupungua kwa idadi ya wahamiaji na wakimbizi wanaongia Ulaya, IOM imetoa mfano wa Italia ikisema mwaka huu imepokea chini ya watu 17,000 ambapo kwa zaidi ya miaka minne iliyopita imekuwa ikipokea wastani wa watu 156,000 kila mwaka.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter