Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yapendekeza dawa ya Dolutegravir (DTG) katika mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI

Kijana barubaru akifanyiwa vipimo vya Virusi vya UKIMWI huko nchini Ivory Coast
UNICEF/Frank Dejongh
Kijana barubaru akifanyiwa vipimo vya Virusi vya UKIMWI huko nchini Ivory Coast

WHO yapendekeza dawa ya Dolutegravir (DTG) katika mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI

Afya

Kwa kuzingatia ushahidi mpya uliotathimini faida na hatari, shirika la afya duniani, WHO,  katika mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI, VVU, hii leo mjini Mexico City huko Mexico, limependekeza matumizi ya dawa za Dolutegravir (DTG) kama njia ya kwanza na ya pili ya matibabu inayopendekezwa kwa watu wote wakiwemo wanawake wajawazito na wale wenye uwezekano wa kupata ujauzito.

Utafiti wa awali ulikuwa umeonesha kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa uhusiano kati ya dawa hiyo ya DTG na tatizo la uti wa mgongo na ubongo ambalo linasababisha watoto kuzaliwa na matatizo kama vile tatizo la mgongo wazi pindi mwanamke anapopata ujauzito akiwa katika matumizi ya dawa.

Tatizo hilo liliripotiwa mwezi Mei mwaka 2018 kutoka katika utafiti uliofanyika nchini Botswana na kukuta visa vine vya matatizo hayo kati ya wanawake 426 ambao walipata ujauzito wakati wakimeza dawa hizo za DTG. Kufuatia utafiti huo wa awali, nchi nyingi ziliwashauri wanawake wajawazito na wanawake wenye uwezekano wa kubeba ujauzito, kumeza dawa za efavirenz (EFV) badala ya DTG.

Hata hivyo data kutoka katika majaribio ya kisayansi ya kulinganisha ufanisi na usalama kati ya DTG na EFV barani Afrika, sasa zimeongeza kiwango cha ushahidi kuwa hatari ya kupata tatizo la uti wa mgongo la ubongo ni ndogo kuliko zilivyokuwa zimekadiriwa awali.

Imeonekana sasa kuwa DTG ni dawa ambazo zina ufanisi zaidi, rahisi kumeza na zina madhara machache kuliko dawa nyingine ambazo zinatumika hivi sasa. DGT pia ina uwezekano mdogo wa kutengeneza usugu wa dawa. Katika mwaka wa 2019, nchi 12 kati ya nchi 18 zilizofanyiwa utafiti na WHO, zilionesha kiwango cha usugu wa dawa za awali kuzidi asilimia zinaazotakiwa yaani 10.

Sababu zote hizo ndio matokeo ya uamuzi wa kuboresha miongozo ya mwaka 2019.

Kwa mwaka huu wa 2019, nchi 82 za kipato cha chini na cha kati ziliripoti kuhama kwenda kaatika matibabu ya VVU yanayotumia DTG. Mapendekezo mapya yaliyoboreshwa yanalenga kusaidia nchi zaidi kuboresha sera zao za kupambana na VVU.

WHO inasema kama zilivyo dawa nyingine, chaguo baada ya kupata ufahamu ni muhimu. Kila maaamuzi ya matibabu yanahitaji ufahamu hasa wa watoa huduma kupima faida na uwezekano wa hatari.

WHO pia inasisitiza umuhimu wa kutoa taarifa na machaguo ya kuwasaidia wanawake kufanya machaguo sahihi.

Kwa hivyo, WHO imetayarisha kikundi cha ushauri wa wanawake wanaoishi na VVU kutoka katika Nyanja mbalimbali ili kusaidia ushauri katika masuala ya sera zinazohusiana na afya zao, ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi. 

WHO inasisitiza haja ya kufuatilia wakati wote hatari za matatizo ya uti wa mgongo na ubongo zinazohusishwa na DTG.