Ubaguzi na unyanyapaa vinaendelea dhidi ya wenye VVU:ILO

26 Julai 2018

Ingawa hatua kubwa zilizopigwa katika kuwatibu watu wanaoishi na virusi vya ukimwi au VVU zimewawezesha kufanya kazi , lakini wanaendelea kubaguliwa kazini umesema utafiti mpya uliozinduliwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani ILO.

Ripoti ya utafiti huo iliyopewa jina “Unyanyapaa na ubaguzi dhiti ya wenye VVU katika ulimwengu wa kazi” imetokana na utafiti uliofanyika katika nchi 13 duniani kwa kuwahoji watu zaidi ya 100,000 wanaoishi na VVU.

Mkuu wa kitengo cha ILO kinachohusika na masuala ya jinsia, usawa, na ukimwi, Shauna Olney akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesema “inasikitisha kuona kwamba licha ya kazi kubwa iliyofanyika kwa miaka mingi bado ubaguzi na unyanyapaa unaendelea.”

Ameongeza kuwa “matibabu pekee hayatoshi , ni lazima tuongeze bidi kupunguza ubaguzi na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU katika mahali pa kazi kwani wana haki ya kufanya kazi na hakuna anayepaswa kuwanyima haki hiyo.”

Matumaini yapo: mtoto huyo amezaliwa bila ukimwi licha ya mama yake kuambukizwa. Picha ya UNICEF/HIVA2015–00099/Schermbrucker
Matumaini yapo: mtoto huyo amezaliwa bila ukimwi licha ya mama yake kuambukizwa. Picha ya UNICEF/HIVA2015–00099/Schermbrucker

 

Ripoti hiyo ambayo imeandikwa kwa ushirikiano na Mtandao wa Kimataifa wa watu wanaoishi na VVU, imezinduliwa katika Mkutano wa kimataifa wa ukimwi “AIDS 2018”,ambao umekuwa ukiendelea kwa juma zima. Huu ni  mkutano mkubwa kabisa wa kimataifa kuhusu masuala ya afya au maendeleo duniani.

Takwimu za ripoti hiyo zinaonyesha kwamba nchi 10 kati ya 13 zimeorodhesha asilimia 30 au zaidi ya kiwango cha ukosefu wa ajira kwa watu wanaoishi na VVU na kiwango kikubwa zaidi kipo miongoni mwa vijana.

Na miongoni mwa wanawake wanaoishi na VVU nafasi yao ya kuajiriwa ni ndogo zaidi kuliko ya wanaume wenye hali kama yao kwa sababu ya majukumu ya bila malipo waliyonayo na kutokuwa na kipato cha kujitegemea.

Zaidi ya hapo utafiti umeonyesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kwa watu waliobadili jinsia, kiko juu katika nchi zote. Olney amesema ripoti hii inacho onyesha ni kwamba bado kuna safari ndefu ili kukomesha unyanyapaa na ubaguzi katika mahali pa kazi kwa watu wanaoishi na VVU.

Ameongeza kuwa hali hiyo imewafanya watu wengi kusita kuweka bayana hali yao ya maambukizi kwa waajiri wao au hata kwa wafanyakazi wenzao.

Pia amesema kuishi na VVU ni sababu nyingine kubwa kwa watu kutopanda cheo makazini . Hivyo amesisitiza kwamba mustakhbali bora kwa watu wanaoishi na VVU hauwezi kupatikana bila kukomesha kwanza ubaguzi na unyanyapaa katika mahali pa kazi.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter