Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto ya ajira kwa vijana Zimbabwe yapata muarobaini kwa msaada wa ILO

Harakati za kilimo na ufugaji zikiendelea barani Afrika.
©FAO/Gustave Ntaraka
Harakati za kilimo na ufugaji zikiendelea barani Afrika.

Changamoto ya ajira kwa vijana Zimbabwe yapata muarobaini kwa msaada wa ILO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Zimbabwe asilimia 70 ya wakazi milioni 13 wa taifa hilo ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 30 ambapo vijana wanne kati ya watano hawana ajira na sasa Umoja wa Mataifa umechukua hatua kuwanusuru.

Takwimu hizo zimechapishwa na shirika la kazi duniani, ILO kupitia video yake ni taswira ya Zimbabwe na nchi nyingi hususan barani Afrika.

Hata hivyo kwa kutambua changamoto ambazo vijana wanakumbana nazo katika harakati zao za kusaka ajira, ILO imetoa mafunzo kwa vijana kwa ajili ya kuwawezesha kuajiriwa lakini pia kujiajiri kwani kabala ya amfunzo hayo hali ilikuwa mbaya kama anavyosimulia mnufaika wa mafunzo huyu.

(Sauti ya mnufaika)

“Kabla ya kuanza mafunzo ya ILO nilikuwa tu nyumbani nakaa”

Kwa upande wake mwakilishi wa ILO nchini Zimbabwe anakiri kwamba changamoto ya ajira kwa vijana si ya nchi hiyo pekee.

(Sauti ya Alphonse Tabi-Abodo)

“Ukosefu wa ajira ni changamoto inayokabili nchi nyingi ikiwemo Zimbabwe, hii imekuwa ni kipaumbele cha mipango ya maendeleo katika nchi nyingi na hata duniani kote kama unavyofahamu mwaka huu ni wa vijana kwenye Umoja wa Mataifa na moja ya changamoto inayokabili vijana ni suala la ajira.”

Miradi ya ILO na wadau inalenga vijana walioko vijijini na hata mijini kwani mazingira yao ni tofauti huku vijana wakipokea mafunzo ya kubuni biashara, kufikia soko na hata kupata stadi ambazo zinawawezesha kuajiriwa. Eunice Matemba ni mmoja wa vijana waliopokea mafunzo na sasa anamiliki saluni ya nywele ambapo anasema

(Sauti ya Eunice)

“Kabla ya kupokea mafunzo ya kutengeneza nywele maisha yangu yalikuwa magumu sana, nilikuwa tu nyumbani huku nikigombana na mume wangu mara kwa mara kwa sababu hela zilikuwa kidogo. Nilikuwa nina mahitaji binafsi ambayo mume wangu alikuwa akisema hela hazitoshi lakini kufuatia mafunzo ya ILO ya saluni ya nywele maisha yangu yamebadilika sasa naweza kukidhi mahitaji ya familia yangu.”

Kitu kinachowezesha mradi huu kufanikiwa ni kwamba fursa ya kiuchumi zinagunduliwa kabla ya mafunzo na hivyo mafunzo yanatolewa kwa vijana katika muda na mazingira waliko vijana.