Ujumbe wa ngazi ya juu wa UN na EU wawasili Mali, hali Mopti si shwari

19 Juni 2019

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix amewasili nchini Mali kwa ziara ya pamoja ya ngazi ya juu akiambata na Naibu Katibu Mkuu wa masuala ya usalama kwenye Muungano wa Ulaya Pedro Serrano, kwa malengo kadhaa ikiwemo kuchagiza utekelezaji wa makubaliano ya amani

Ziara yao ya siku tatu inafanyika wakati mashambulizi dhidi ya raia yakiendelea kwenye maeneo ya kati mwa nchi hiyo hususan  kwenye jimbo la Mopti lililopo mpakani na Burkina Faso.

Mashambulizi hayo ni pamoja na ya juzi Jumatatu ambapo watu walio na silaha walivamai vijiji vya Yoro na Gangafani ambapo taarifa za awali zinasema watu 38 waliuawa na wengine wengi walijeruhiwa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari kuwa punde baada ya shambulio hilo, vikosi vya ulinzi na usalama nchini Mali vilipelekwa eneo hilo ili kuimarisha usalama na kuchunguza mashambulio hayo.

Amemnukuu tena Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye anataka kukomeshwa kabisa kwa mwendelezo huo wa mashambulizi dhidi ya raia nchini Mali na wahusika wafikishwe mbele ya sheria na suala la maridhiano na amani lipatiwe kipaumbele.

Ni katika muktadha huo akiwa ziarani Mali, Bwana Lacroix na Bwana Serrano watakutana na viongozi wa Mali na wadau wengine muhimu kuangalia jinsi ya kuimarisha msaada wa Umoja wa Mataifa na EU katika kusongesha mkataba na kurejesha mamlaka za serikali kwenye maeneo ya kaskazini na kati mwa Mali.

Halikadhalika kuimarisha ubia kati ya vyombo hivyo viwili.

Lacroix na Serrano watakutana na viongozi wa ngazi ya  juu wa serikali ya Mali, vikundi vilivyojihami ambavyo vilitia saini makubaliano ya amani, wawakilishi wa kisiasa na mashirika ya kiraia, vikundi vya wanawake na wadau wa kimataifa.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter