Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko yenye mlengo wa kijamii Mopti Mali yatutia hofu:UN

Moja ya vijiji kwenye eneo la Mopti nchini Mali.
WFP/Alexandre Brecher-Dolivet
Moja ya vijiji kwenye eneo la Mopti nchini Mali.

Machafuko yenye mlengo wa kijamii Mopti Mali yatutia hofu:UN

Amani na Usalama

Machafuko yenye mwelekeo wa kijamii yanayoendelea katika jimbo la Mopti katikati mwa nchi ya Mali yanatia wasiwasi mkubwa kwa mujibu wa ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis, ofisi hiyo imesema katika wiki za karibuni wafanyakazi wake nchini Mali wameorodhesha mwenendo wa raia kufurushwa makwao ama baada ya kulengwa moja kwa moja, kwa sababu ya jamii wanazotoka au baada ya mashambulizi yaliyosababisha vifo kwa watu wa jamii zao katika vijiji vya jirani. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Geneva

(SAUTI YA RUPERT COLVILE)

“Tangu mwanzoni mwa mwaka huu ofisi ya haki za binadamu na idara ya ulinzi ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, wameorodhesha matukio 99 ya machafuko ya kijamii yaliyosababisha takriban vifo 289 vya raia. Matukio 76 sawa na asilimia 77 ya matukio yote yametokea jimbo la Mopti pekee, 49 kati ya hayo ni ya tangu Mei Mosi.”

Ameongeza kuwa wanaipongeza serikali ya Mali kwa juhudi ambazo tayari imeshazichukua kuingilia kati mzunguko wa machafuko hayo hususan jimboni Mopti na wameitaka kuendelea kuchukua hatua ikiwemo zinazotekelezwa na vikosi vya serikali na kulichukulia suala hili kama suala la dharura.