Kuchafua hali ya hewa ni kujichimbia kaburi

5 Juni 2019

Leo ikiwa ni siku ya mapumziko kwenye Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Siku kuu ya Eid, tuna Jarida Maalum likiangazia siku ya mazingira duniani, mwaka hii mwelekeo ukiwa ni uchafuzi wa hewa. Darubini zimeanza nchini Kenya, kisha Tanzania na kuhitimisha Uganda, msimulizi wako ni Assumpta Massoi.

 

Maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya mazingira duniani yakiangazia uchafuzi wa hewa yamebeba kauli mbiu, “pambana na uchafuzi wa hewa’ ikiwa ni wito wa kukabiliana na janga hilo linaloikabili Dunia. Kwanza kabisa tunaanzia nchini Kenya ambako tunasikia maoni ya waendesha magari ya usafiri wa umma almaarufu matatu walipohojiwa na mwandishi wetu nchini Jason Nyakundi, mjini Nairobi.

Pamoja na maoni ya wananchi tumeangazia je serikali ya Kenya kupitia mamlaka ya kitaifa ya kusimamia mazingira, NEMA inafanya nini sio tu kudhibiti lakini kuhakikisha hewa safi na ulinzi wa mazingira? Tumezungumza na Evans Nyabuto mkurugenzi wa mawasiliano, NEMA kuhusu mikakati yao ya kuhakikisha hewa safi lakini pia changamoto.

Julius Mwelu/UN-Habitat
Sehemu ya mji wa Nairobi ambako kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa unaosababishwa na Matatu, watu wanaweza kuathiriwa afya zao.

Kwa upande wake, Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Alvaro Rodriguez amesema licha ya kwamba suala la uchafuzi wa hewa halizungumziwi ipasavyo lakini athari zake ni dhahiri.

Bwana Alvaro amesema kuwa "Umoja wa Mataifa kwa pamoja na nchi wanachama, wamekubaliana kwamba uchafuzi wa hewa ni muhimu na ni lazima ijadiliwe kama sehemu ya maendeleo ya kila nchi, na haswa ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu na hata takriban nchi 155 zinataja mazingira safi kama haki ya kikatiba kwa raia wake.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud