Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa FAO wa kusambaza mbegu bora Kenya wamwezesha kijana kujitegemea

Miradi ya FAO ya kuwawezesha wakulima kama hawa kupata stadi za kilimo bora, inaongeza uzalishaji na  hivyo kuinua kipato cha wakulima.
UNDP Uganda/Luke McPake
Miradi ya FAO ya kuwawezesha wakulima kama hawa kupata stadi za kilimo bora, inaongeza uzalishaji na hivyo kuinua kipato cha wakulima.

Mradi wa FAO wa kusambaza mbegu bora Kenya wamwezesha kijana kujitegemea

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mpango wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO nchini Kenya wa kuwapatia mbegu za kisasa wakulima walioathiriwa na mafurikio kwenye kaunti ya mto Tana mwaka jana umeleta mafanikio makubwa siyo tu kwa lishe bali pia kipato.

Ni Hiribae Dulu, mkulima kijana mwenye familia ya mke na watoto watatu amekuwa mkulima huko eneo la Idsowe kaunti ya mto Tana nchini Kenya tangu mwaka 2016, ambapo mwaka jana zahma  ya mafuriko ya kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2018 ilisomba mazao yaliyokuwa tayari kuvunwa.

FAO kufuatia ombi la serikali ya Kenya ikawapatia mbegu bora ili maji yaliyotwama yakiondoka waweze kupanda na kujipatia kipato,  mbegu hizo ni pamoja na zile za mahindi zinazokomaa baada ya miezi miwili ambapo Hiribae anasema kwamba, "tulipopewa mbegu  hizi tukapewa mbegu za mahindi kilo nne, mbegu za pojo kilo nne,  tukapewa mbegu za kunde pia kilo nne, na tukapewa gramu 100 za sukumawiki.  imenisaidia sukumawiki, imenisaidia mahindi na kwanza  tunapoongelea mahindi, yako na afya nzuri na yanazaa  mahindi mawili mawili , matatu hadi manne na hii ni faida sana kwetu sisi wakulima."

Kijana huyo anasema kuwa mboga za majani alizovuna zinatumika pia kwa matumizi ya nyumbani na hivyo kuokoa fedha ambazo angalitumia kwa ajili ya manunuzi ya mboga na ametoa wito kwa vijana wenzake washiriki kwenye kilimo kwa kuwa kinasaidia kuongeza kipato na kuinua ustawi.

Hiribae anasema tangu aanze shughuli za kilimo mwaka 2016 ameweza kujitegema na kujilipia mafunzo ya diploma na kwamba kwa mapato aliyopata baada ya mauzo ya mavuno ya mbegu za FAO anapanga kujilipia masomo ya shahada ya uzamili hivyo ametoa wito kwa wadau akisema kwamba, "labda kama ningeomba washika dau kama vile serikali za kaunti au serikali kuu wafungue vyuo vya mafunzo ya stadi au Polytechnics kwa wingi na wapatie walimu na vifaa vinavyohusiana na kilimo ili kusaidia idadi kubwa ya vijana wetu walio majumbani na hawana shughuli ya kufanya."

FAO inasema kuwa kwa kuwekeza kwa vijana, inawawezesha kuchukua hatua na kuwa sehemu ya lengo malengo endelevu, SDGs la kutokomeza njaa duniani ifikapo mwaka 2030.