Mafunzo ya FAO yaleta nuru kwa mkulima mwenye umri wa miaka 63 Tanzania

6 Septemba 2019

Nchini Tanzania mkulima mmoja mwenye umri wa miaka 63 kwa mara ya kwanza amenufaika na shughuli za kilimo baada ya kupatiwa mafunzo yaliyoratibiwa na shirika la chakula na kilimo FAO nchini  humo. 

Yohana Zablon mkazi wa kijiji cha Njage mkoani Morogoro, nchini Tanzania anasema kwa miaka yote amekuwa akilima kwa kutumia stadi za kienyeji.

Hata hivyo miezi michache iliyopita alifuatwa na kikundi cha vijana cha Tupendane waliokuwa wamepatiwa mafunzo ya kilimo cha mpunga, mafunzo yaliyoandaliwa na FAO kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo nchini humo, ambapo alishiriki kwenye mashamba darasa.

Vijana hao walipatiwa mafunzo na stadi ya kuongeza mavuno kwa kutumia kiwango kidogo cha maji, eneo dogo la shamba na kiwango kidogo cha mbegu.

Zablon anasema, “hawa vijana walinifundisha jinsi ya kuchagua mbegu, kuanzisha kitalu cha mbegu na muda mzuri wa upanzi. Pia walinielekeza jinsi ya kuweka nafasi kati ya shimo la mbegu moja na nyingine na sasa huyu ndio Zablon mpya, hawa vijana wanazalisha kwa tija na nawasikiliza.”

Kwa sasa Zablon ameongeza uzalishaji kutoka magunia 15 hadi 40 kwa ekari moja.

Katibu wa kikundi cha Tupendane Samuel Mwangata amempongeza Zablon na wakulima wengine vijana kwa kuonyesha ari yao na kwamba, “Zablon na wakulima wengine tuliowajumuisha kwenye kikundi katu hawakosi mafunzo na wana ari ya kujifunza mbinu mpya za kuboresha kilimo.”

Hivi sasa kikundi cha Tupendane kina wanachama 25 ambao kwa pamoja wanamiliki ekari 4 za mashambab darasa na pia wamesajili wakulima wengine 100 vijana na 25 watu wazima kutoka kijiji cha Njage.

Kwa mujibu wa FAO lengo ni kutumia mradi huo kutokomeza njaa ambayo ni lengo namba 2 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud