Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tsunami ni ‘mwiba’ kwa uhai wa binadamu na uchumi wa nchi- UNISDR

Kijiji kimoja  katika kisiwa chaSulawesi, Indonesia kiliharibiwa kabisa.Wakati tetemeko la ardhi lilipotokea watu walikimbilia kwenye bahari  wakiogopa nyumba zao zitawangukia. Tena tsunami ikafuatia.
OCHA/Anthony Burke
Kijiji kimoja katika kisiwa chaSulawesi, Indonesia kiliharibiwa kabisa.Wakati tetemeko la ardhi lilipotokea watu walikimbilia kwenye bahari wakiogopa nyumba zao zitawangukia. Tena tsunami ikafuatia.

Tsunami ni ‘mwiba’ kwa uhai wa binadamu na uchumi wa nchi- UNISDR

Tabianchi na mazingira

Hii leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kuelimisha jamii  kuhusu tsunami, msisitizo ukiwa ni  hasara za kiuchumi, Umoja wa Mataifa unasema idadi ya vifo na hasara za kiuchumi zitokanazo na matukio ya tsunami kwa nchi zinazopakana na bahari ya India na Pasifiki zimeongezeka katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Tathmini ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza hatari za majanga, UNISDR imesema katika kipindi hicho watu 251,770 walipoteza maisha kutokana na tsunami ilhali hasara ya kiuchumi ilikuwa dola bilioni 280.

Ofisi hiyo imesema kiwango hicho ni cha juu ikilinganishwa na vifo 998 na hasara ya dola bilioni 2.7 kwa miongo miwili ya awali yam waka 1978 hadi 1997.

Akifafanua kwa kina kuhusu takwimu hizo, afisa mawasiliano wa UNISDR, Janet   Erthworth ametaja sababu za ongezeko kuwa ni tsunami ya disemba 2004 na ile ya mwaka 2011 huku akisema..

“Kwa hiyo matukio haya mawili ya wakati tofauti yanatukumbusha kuwa tsunami, licha ya kwamba hutokea mara chache, ni janga linalosababisha  vifo vingi na hasara kubwa zaidi kuliko majanga mengine. Kwa hiyo cha kufanya , UNISDR kwa mujibu wa mpango wa Sendai inajikita kwenye mifumo ya kutoa maonyo mapema, mipango ya kitaifa ya kupunguza hatari za majanga na pia mipango ya kuelimisha umma. Hatuwezi kutegemea sana teknolojia  yake, kwa hiyo tunahitaji kujumuisha jamii.”

Siku hii inaadhimishwa wakati jimbo la Sulawesi Kati nchini Indonesia bado linajikwamua kutoka katika athari za tetemeko la ardhi na tsunami vilivyokuba nchi hiyo tarehe 28 mwezi Septemba mwaka huu.

Tsunami hutokea baada ya tetemeko la ardhi kukumba eneo ndani ya baharí na hivyo kusababisha mawimbi makubwa ya maji yanayoenda kwa kasi kubwa hadi nchi kavu.