Mradi wa FAO wa kutakatishamajitaka ni muarobaini wa kupunguza visa vya kipindupindu Yemen

26 Agosti 2019

Nchini Yemen mradi wa pamoja wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO na serikali ya Japan umesaidia wakulima kupata maji salama kwa ajili ya kumwagilia mboga za majani na hivyo kuondokana na visa vya kipindupindu.

Ukosefu wa miundo mbinu ya maji, kukauka kwa na mifumo mibovu ya maji taka inafanya watu wengi nchini Yemen watumie maji yasiyo salama.

Kupitia video ya shirika la chakula na kilimo duniani, FAO tunakutana na mkulima Adba Mubarak mwenye umri wa miaka takriban sitini akiwa eneo la Bani Al Hareth, Sana’a yeye ni miongoni mwa watu wanoutumia maji yasiyo salama ambayo yanasababisha magonjwa kama vile kipindupindu. Bi. Mubarak anasema,

(Sauti ya Bi Mubarak)

“Tulitumia majitaka kumwagilia mboga, niliugua sana, sikuweza kutembea, sikuwa na uwezo wa kusonga. Sasa hivi majitaka hayo yametakatishwa na watu hawaugui kipindupindu tena na kufa.”

Wakulima licha ya kutambua hatari za kutumia maji taka hayo walihisi kama hawakuwa na njia mbadala na ari  ya kulima mazao ilikuwa kubwa sana kiasi cha kuhisi hawana namna.

FAO kwa ushirikiano na Japan kwa kuona changamoto hiyo wamekuja pamoja na umoja wa watumiaji wa maji na kuweka vituo vya kutakatisha maji, vituo  ambavyo vinatoa maji salama kwa ajili ya matumizi ya kilimo.

Mradi huu unahakikisha kwamba wakulima wa Yemeni ambao hulima kila siku kwa ajili ya kulisha familia zao wanaweza kufanya hivyo bila hatari ya kipindupindu.

Wanakijiji pia wanaelimishwa kuhusu umuhimu wa kutumia maji safi na kuzingatia usafi na kusaka matibabu pindi tu wanapohisi kuugua. Walid Saleh ni mshauri mkuu wa kiufundi, FAO.

(Sauti ya Walid Saleh)

“Tunafuraha hapa FAO na Yemen kwa kuzinduliwa kituo cha kutakatisha maji katika eneo la Bani Al Hareth karibu na mji wa Sana’a kukabiliana na tatizo la majitaka ambayo wanatumia kwa umwagiliaji hali ambayo iliongeza visa vya kipindupindu. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 45 ya visa vya kipindupindu vinatokana na matumizi ya vyakula vichafu. Uwepo wa kituo hiki utawezesha wakulima wadogowadogo kutumia maji safi.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter