Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msumbiji ilinde wazee dhidi ya ukatili hususan wakati wa dharura- Mtaalam huru UN

 Rosa Kornfeld-Matte Mtaalam maalum kuhusu wazee kufurahia haki zote za binadamu
Picha ya UN/Jean-Marc Ferré
Rosa Kornfeld-Matte Mtaalam maalum kuhusu wazee kufurahia haki zote za binadamu

Msumbiji ilinde wazee dhidi ya ukatili hususan wakati wa dharura- Mtaalam huru UN

Haki za binadamu

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa aliyeko ziarani Msumbiji amepongeza serikali ya nchi hiyo kwa juhudi zake na dhamira ya kuweka sera na sheria za kuhakikisha wazee wanafurahia haki zao huku akisisitiza utekelezaji unahitajika. Akizingatia hali ya dharura ya sasa kutokana na vimbunga Idai na Kenneth, mtaalamu huyo ametoa wito kwa mamlaka kuhakikisha wazee wanalindwa kutokana na ukatili na unyanyasaji.

Kupitia taarifa ya ofisi ya haki za bindamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, mtaalamu huyo  Rosa Kornfeld-Matte amesema makadirio ya ongezeko la idadi ya wazee kwenye nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara linakadiriwa kuwa la kasi ya haraka kuliko ukanda mwingine na hivyo changamoto zinazotokana na hali hiyo ni pana na wazi.

Licha ya kwamba mtaalam huru huyo amefanya ziara yake kutathmini haki za wazee lakini ziara hiyo imekuja wakati huu ambapoMsumbiji imepigwa na kimbunga Kenneth, wiki sita tu baada ya kupigwa na kimbunga Idai na kwa hivyo ameelezea mshikamano wake na Msumbiji huku akielezea kusitkitishwa na vifo na wakati huo huo kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kujitoa kwa hali na mali kukabiliana na mahitaji ya sasa nay a muda mrefu.

Halikadhalika Bi. Kornfeld-Matte ameshauri serikali kutekeleza mapendekezo ya kulinda wazee ikiwemo, mkakati wa malipo ya uzeeni, mgao kwa wazee na sheria ya kulinda haki za wazee ni hatu kubwa iwapo itatekelezwa.

Msumbiji inakabiliwa na changamoto nyingi za kiafya ikiwemo Virusi Vya Ukimwi, VVU na Ukimwi ambapo kwa hilo amepongeza serikali kwa juhudi zake katika kulinda wazee.

Aidha katika kushughulikia wazee ameongeza kuna suala la umaskini na umaskini wa watoto kwani wazee wengi ni walezi wa watoto yatima na waliohatarini kutokana na VVU na  Ukimwi kwa hivyo gharama ya huduma ya afya ni ya juu kwa wazee.

Mtaalam huru huyo amesema kiwango kikubwa cha umaskini miongoni mwa wazee ikiwa ni asilimia 23 na unyanyasaji kiuchumi wanokabiliwa nao wazee ni moja ya maeneo yanayotia wasiwasi huku wazee wakitengwa, kunyimwa haki ya makazi, ardhi, mali na msaada wakijamii, malipo ya uzeeni na matumizi mabaya ya mbinu za kujipatia kipato.

Bi. Kornfeld-Matte, pia ameelezea kushtushwa na madai ya vitendo vya uchawi dhidi ya wazee hususan wanawake akisema vinatumika kuhalalisha ukatili na kutelekezwa na hata mauaji.

Kwa mantiki hiyo ametaka hatua kuchukuliwa kutokomeza hali hiyo.

Mtaalam huru huyo amesema kuenea kwa vitendo vya ukatili ni ishara kwamba hatua za hivi sasa hazifai na hatua madhubuti zinahitajika kutambua, kuripoti na kuzuia aina zote za ukatili wa wazee, kuwalinda na kuhakikisha ulinzi dhidi ya kunyanayswa kuchumi na aina zaingine za unyanyasaji, ukatili na kutesswa.

Wakati wa ziara yake bi. Kornfeld-Matte ametembelea Maputo, Beira, Chimoio, Manica na Sofala na kukutana na wawakilishi mbali mbali wa serikali,mashirikia ya kibinadamu, mashirikia ya kiraia na baadhi ya watu watetezi wa haki za wazee na watu wazee wenyewe.

Mtaalam huru huyo atawasilisha ripoti yake kwenye Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Septemba mwa huu wa 2019.