Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takribani watu milioni 1.9 hawatokuwa na chakula Msumbiji wakati wa msimu wa muambo:WFP

Vimbunga Idai na Kenneth nchini Msumbiji vimeacha wananchi wengi taabani
UN/Eskinder Debebe
Vimbunga Idai na Kenneth nchini Msumbiji vimeacha wananchi wengi taabani

Takribani watu milioni 1.9 hawatokuwa na chakula Msumbiji wakati wa msimu wa muambo:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Ripoti iliyotolewa karibuni inayoelezea hali ya uhakika wa chakula nchini Msumbiji (IPC) inaonesha kuwa baada ya kukumbwa na vimbunga viwili zaidi ya watu milioni 1.6 wako katika hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula katika kiwango cha daraja la 3 au zaidi katika wilaya 63 ambazo zimefanyiwa tathimini.

 Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema kuwa zaidi ya watu 188,000 kati ya watu zaidi ya milioni 29 nchini humo  wako katika daraja la nne la uhaba wa chakula, daraja ambalo ni baya zaidi.

Ripoti ya IPC inatambulika na kukubalika kimataifa na hutoa muongozo wa viwango mbalimbali vya kutokuwa na uhakika wa chakula na kuzisaidia nchi na wadau wa misaada kuchukua hatua za kuokoa maisha kabla hali haijawa mbaya zaidi.

WFP imesema inatarajiwa kwamba katika msimu wa muambo ambao utaanza Oktoba mwaka huu hadi Machi mwaka 2020 hali itakuwa mbaya zaidi a,mbapo “watu zaidi ya milioni 1.9 watakuwa katika daraja la 3 la mgogoro wa chakula au zaidi endapo hakutokuwa na msaada wa kibinadamu.“

Ikiwa ni  miezi mne baada ya Idai, eneo la pwani la mji wa Beira bado linajikwamua na athari za kimbunga hicho
UN Mozambique
Ikiwa ni miezi mne baada ya Idai, eneo la pwani la mji wa Beira bado linajikwamua na athari za kimbunga hicho

Hivi sasa mkakati wa kuchukua hatua kukabilkiana na hali hiyo unafanyiwa kazi ili kuhakikisha unakidhi mahitaji. Tayari mipango ya WFP ni kuwasaidia watu zaidi ya 560,000 kwa mwezi tangu mwezi huu wa Julai hadi Oktoba hususan walioathirika na vimbunga lakini pia maeneo yaliyoathirika na ukame.

“Na wakati mahitaji yakiendelea kuongezeka WFP inatarajia kuongeza msaada hadi kwa watu milioni 1.25 kwa mwezi wakati wa msimu wa muambo kuanzia Oktoba mpaka Machi 2020 endapo fedha za ufadhili zitakusanywa kwa wakati muafaka. Watu 900,000 watakaosaidiwa katika mpango huo ni wale walioathirika na kimbunga Idai, 100,000 katika maeneo yaliyoathirika na kimbunga Kenneth na wengine 250,000 ni katika maeneo yaliyoathirika na ukame.”

WFP inasema ili iweze kutoa msaada unaohitajika kwa wakati nchini Msumbiji kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka rasilimali fedha lazima zikusanywe na kupatikana sasa, na shirika hilo linahitaji dola milioni 102 kwa ajili ya mahitaji ya miezi sita ijayo.