Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kama maisha hayakupi maana, ala za jazz zitafanya kazi hiyo-Azoulay

Antonio Sanchez, mwanamuziki wa muziki aina ya Jazz na mshindi wa tuzo ya Gramy.
Justin Bettman
Antonio Sanchez, mwanamuziki wa muziki aina ya Jazz na mshindi wa tuzo ya Gramy.

Kama maisha hayakupi maana, ala za jazz zitafanya kazi hiyo-Azoulay

Utamaduni na Elimu

Muziki wa Jazz unaelezea maisha na una jukumu muhimu la kuchagiza amani, majadiliano na kuyafanya maisha yawe na maana muhimu kwa watu wote duniani, amesema mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sanyansi na utamaduni UNESCO katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya muziki wa Jazz hii leo.

Katika ujumbe wake maalum mkurugenzi huyo wa UNESCO Audrey Azoulay amenukuu kauli ya hayati Dkt. Martin Luther King Jr aliyoitoa kwenye tamasha la Jazz mwaka 1964 mjini Berlin Ujerumani na kusema”wakati maisha yenyewe hayakupi muongozo wala maana yoyote wanamuziki wa jazz wanaunda muongozo huo na kukupa maana kupitia vyombo vyao vya muziki.”

Ameongeza kuwa uhuru na uwazi ndio kiini cha muziki wa Jazz unaotoa fursa ya kukumbatiwa na tamaduni zote ulimwenguni, ukiwapa matumaini na sauti mamilioni ya watu wanaohangaika na kuwa kama nembo muhimu ya uhuru wa kujieleza na utu wa binadamu na ndio maana Jazz inaheshimika kwa kuchagiza majadiliano na amani husuan katika wakati huu ambao kuna ongezeko kubwa la mgawanyiko duniani.

Antonio Sanchez mwenye asili ya Mexico ni gwiji wa muziki wa Jazz hapa nchini Marekani, akizungumza na UN News ameunga mkono kauli hiyo

(SAUTI YA SANCHEZ)

“Jazz ni mfumo wa sanaa ulio jumuishi, ambayo inachukua vingele vingine muhimu na kuvitumbukiza katika muziki. Hivyo kwangu mimi maana ya Jazz ni uhuru, kama mwanamuziki inanipa uhuru wa kujieleza vile ninavyohisi kwa siki hiyo na wakati huo.”

Na uhuru huo ndio anaousisitiza mkurugenzi mkuu wa UNESCO Azoulay na kutoa wito kote duniani kwamba “tunapoadhimisha siku hii hebu tuongozwe na maadili na mtazamo wa Jazz kama jeshi moja na sauti ya uhuru na matumaini ya watu wote duniani.”

Kimataifa siku hii inasherehekewa nchini Australia ikiambatana na tamasha maalum la muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali mashuhuri wa Jazz akiwemo balozi mwema wa UNESCO na miongoni mwa waliopigia upatu kuanzishwa kwa siku ya Jazz duniani Herbie  Hancock.