Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunachukua hatua lakini ukatili wa kingono bado umeota mizizi- Guterres

Manusura wa ubakaji nchini Sudan Kusini akisimulia kisa kilichompata. Alitoa simulizi hiyo kwenye eneo moja karibu na mji wa Bentiu. (Picha hii ni  ya Desemba 2018)
UNMISS/Isaac Billy
Manusura wa ubakaji nchini Sudan Kusini akisimulia kisa kilichompata. Alitoa simulizi hiyo kwenye eneo moja karibu na mji wa Bentiu. (Picha hii ni ya Desemba 2018)

Tunachukua hatua lakini ukatili wa kingono bado umeota mizizi- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wakati sasa umewadia kuchukua hatua mpya ili kutokomeza ukatili wa kingono kwenye mizozo, wakati huu ambapo vimeshamiri kuanzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Sudan Kusini hadi Myanmar.

Bwana Guterres amesema hayo leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakati akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kiongono, akisema kuwa licha ya hatua zote walizochukua, matukio ya kikatili ya ukatili wa kingono yameendelea kushamiri kwenye mizozo.

Mathalani amesema, “katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yangu nimesikiliza shuhuda za ukatili wa kingono kwenye maeneo ya mizozo kuanzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hadi iliyokuwa Yugoslavia. Huko Bangladesh mwaka jana, wakimbizi wa kabila la Rohingya walinieleza kuhusu vitendo vya ubakaji wa wanawake na wasichana huko nyumbani kabla ya kukimbia Myanmar.”

Baadhi ya wanawake waathirika wa unyanyasaji wa kingono Sudan kusini wakizungumza na viongozi wa Umoja wa Mataifa
UN Photo/Isaac Billy
Baadhi ya wanawake waathirika wa unyanyasaji wa kingono Sudan kusini wakizungumza na viongozi wa Umoja wa Mataifa

Ukatili wa kingono una uhusiano na ubaguzi wa kijinsia

Amesema ni lazima kutambua kuwa “ukatili wa kingono kwenye mizozo kwa kiasi kikubwa unaathiri wanawake na wasichana kwasababu wanahusika moja kwa moja na suala la ukosefu wa usawa wa jinsia na ubaguzi. Kuzuia ni lazima kuzingatie kuendeleza haki za wanwake na usawa wa kijinsia kwenye maeneo yote kabla, wakati na baada ya vita.”

Katibu Mkuu amewaambia wajumbe kuwa ni lazima kutambua uhusiano kati ya ubaguzi wa kijinsia na ukatili wa kingono akisema, “watu wenye misimamo mikali na magaidi mara nyingi hujenga itikadi zao kwenye fikra za ukandamizaji wa wanawake  na wasichana na hutumia ukatili wa kingono kwa njia mbalimbali ikiwemo ndoa za lazima na utumwa.”

Hatua za kuchukua

Bwana Guterres ametaka ujumuishwaji zaidi wanawake kwenye ulinzi na  ujenzi wa amani akisema, “pale ambapo wanawake ni sehemu ya ujumbe wa ulinzi wa amani, tunafahamu kuwa taarifa na ulinzi dhidi ya ukatili wa kingono zinaongezeka. Pale ambapo wanawake wako kwenye meza ya usuluhishi, kuna fursa kubwa zaidi ya uwajibikaji wa vitendo hivyo.”

Halikadhalika Katibu Mkuu amependekeza umuhimu wa kusaidia manusura wa ukatili huo na familia zao ikiwemo kuwapatia huduma za afya, fidia na misaada mingine na ndipo akatoa pongeza kwa Dkt. Denis Mukwege kwa juhudi zake anazofanya huko Bukavu, jimbo la  Kivu Kusini kusaidia wanawake manusura wa ubakaji.

Wanawake wakimbizi wa Rohingya walionusurika  ukatili wa kingono wanatengwa sana na jamii yao kwenye kambi za wakimbizi Bangladesh
UNICEF/Brian Sokol
Wanawake wakimbizi wa Rohingya walionusurika ukatili wa kingono wanatengwa sana na jamii yao kwenye kambi za wakimbizi Bangladesh

“Napongeza juhudi za Dkt. Mukwegeza kuanzisha fuko la kimataifa la kusaidia manusura wa ukatili wa kingono na natoa wito kwa serikali kuchangia ili mfuko huo uweze kubadilisha maisha ya wale ambao wameathirika na pia kuchangia kwenye mikakati inayotakiwa,” amesema Katibu Mkuu.

Guterres amesihi Baraza la Usalama liendele kushirikiana ili kumaliza tofauti kuhusu suala hilo akisema hatua za pamoja kuondokana na uhalifu huo lazima zihakikishe watekelezaji wanaadhibiwa na manusura wanapatiwa msaada wa kutosha huku haki zao za kibinadamu zikilindwa.

“Kwa pamoja, tunaweza kuondoa ukwepaji sheria na kuweka haki na pia kumaliza kutochukua hatua kwa kuchukua hatua,” amehitimisha Katibu Mkuu.

Bora kubakwa na gaidi mmoja wa Boko Haram kuliko kujiuza kila siku ili nilishe wanangu

Katika mkutano huo, Pramila Patten ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili kwenye mizozo alitumia sehemu ya hotuba yake kuelezea simulizi kutoka kwa manusura wa ukatili wa kingono ambao amesema mara nyingi hutumika kama mkakati wa kufukuza jamii fulani au kukwamua rasilimali.

Ametoa mfano huko Cox’s Bazar nchini Bangladesh ambako amesema kuwa "nilikutana na wanawake na wasichana warohingya ambao walielezea mfumo ulioenea wa ukatili ikiwemo ubakaji wa magenge uliofanywa na jeshi kama sehemu ya operesheni ya kuwafurusha warohingya kutoka jimbo la Rakhine.”“Nilikutana na wanawake na wasichana ambao walitoroka Boko Haram. Nikiwa nimekaa nao kwenye chumba kimoja, nilihesabu watoto kadhaa waliokuwa wamewabeba. Nilishtushwa pindi waliponieleza kuwa walikuwa bora zaidi na magaidi wa Boko Haram ambako walibakwa na mtu mmoja kuliko hapo kambini ambako kila siku wanapaswa kuuza miili yao waweze kulisha watoto wao.” Pramila Patten

Bi. Patten amesema huko Iraq ,“nilikutana na wanawake waliotekwa na Daesh wakiwemo wa kabila la Yazidi, Turkmen Shia na wanawake wakristo ambao walikabiliwa na chaguo la kuvunja moyo la waache watoto wao waliozaliwa kutokana na kubakwa ili waweze kukubalika kwenye jamii zao au wasijree nyumbani kabisa kwasababu hawakuwa na uwezo wa kutelekeza watoto wao. Watoto hao ni maelfu kwenye maeneo ya mizozo iliyodumu muda mrefu kama vile Bosnia, Colombia, Syria, Iraq, Pembe ya Afrika, DRC na Afrika Magharibi.”

Tubadili utamaduni wa ukwepaji sheria uwe utamaduni wa uwajibikaji

Kwa mantiki hiyo amesema “iwapo tunataka kuzuia uhalifu kama huu kwanza kabisa tukatae ukweli usiokubalika ya kwamba kumbaka mwanamke, msichana au kumnajisi mtoto kwenye mzozo popote pale duniani hakuna gharama yoyote.

Bi. Patten amesema ili kubadili mwelekeo, lazima kuongeza gharama na athari kwa wale ambao wanatekeleza vitendo hivyo, wanaoagiza vitekelezwe na wale wanaoendekeza vitendo hivyo kwenye mizozo akisema ni “lazima tubadili karne za utamaduni wa ukwepaji sheria kuwa utamaduni wa uwajibikaji.”

Pramila Patten, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili kwenye mizozo wakati akihutubia Baraza la Usalama hii leo Aprili 23, 2019
UN /Loey Felipe
Pramila Patten, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili kwenye mizozo wakati akihutubia Baraza la Usalama hii leo Aprili 23, 2019

Nilipokwenda Maiduguri nchini Nigeria, nilikutana na wanawake na wasichana ambao walitoroka Boko Haram. Nikiwa nimekaa nao kwenye chumba kimoja, nilihesabu watoto kadhaa waliokuwa wamewabeba. Nilishtushwa pindi waliponieleza kuwa walikuwa bora zaidi na magaidi wa Boko Haram ambako walibakwa na mtu mmoja kuliko hapo kambini ambako kila siku wanapaswa kuuza miili yao waweze kulisha watoto wao.  

 

Azimio namba 328 kuhusu ukatili wa kingono lapitishwa

 

Wakati wa mjadala huo wa wazi, Ujerumani iliwasilisha azimio kuhusu ukatili wa kingono kwa lengo la kuhakikisha hatua mujarabu zinachukuliwa kwa ajili ya siyo tu kuzuia ukatili wa kingono bali pia kuwasaidia manusura.

 

Kura zilipopigwa, wajumbe 13 kati ya 15 wanachama wa Baraza la Usalama walipitisha azimio hilo, huku wajumbe wawili Urusi na China hawakupiga kura.

 

Kwa mantiki hiyo azimio hilo limepita na pamoja na mambo mengine linasisitiza kuwa vitendo vya ukatili wa kingono na kijinsia kwenye mizozo viwanaweza kuwa sehemu ya malengo mkakati na itikadi vinavyotumiwa na baadhi ya pande husika kwenye mzozo.

 

Kwa  mantiki hiyo, Baraza kupitia azimio hilo limeazimia kuwa manusura wanapaswa kuwa na fursa ya kupatiwa msaada kupitia mipango ya kitaifa ya usaidizi na fidia pamoja na huduma za afya, kisaikolojia, makazi salama, fursa za kujikwamua kimaisha na msaada wa kisheria, “ na hiyo iwe kwa manusura wote, wanawake, wasichana na watoto waliozaliwa kutokana na vitendo vya ukatili wa kingono pamoja na wanaume na wavulana ambao ni wahanga wa ukatili wa kingono mizozoni, ikiwemo kwa kuswekwa korokoroni.”