Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama latakiwa kushughulikia uhalifu ‘ulionyamaziwa zaidi na unaokemewa kwa kiwango cha chini’

Muathirika wa ukatili wakingono mjini Goma DRC.
Picha ya UN/Marie Frechon (Maktaba)
Muathirika wa ukatili wakingono mjini Goma DRC.

Baraza la Usalama latakiwa kushughulikia uhalifu ‘ulionyamaziwa zaidi na unaokemewa kwa kiwango cha chini’

Amani na Usalama

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Unyanyasaji wa Kijinsia na Migogoro Pramila Patten, leo tarehe 14 Julai ameliambia Baraza la Usalama kwamba "ubakaji wa genge, utumwa wa kingono na aina nyingine za unyanyasaji wa kingono zinatumika kama mbinu ya vita, mateso na ugaidi kutisha na kufurusha watu.” 

Akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza, Patten amesema "kuongezeka kwa majeshi na kuenea kwa silaha kunaleta migogoro kote ulimwenguni kwa kiwango cha juu, na kuunda mazingira ya ukatili usiofikirika na usiokoma." 

Akibainisha kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ndiyo nchi inayowasilisha idadi kubwa zaidi ya natuki ya ukiukaji 701 uliothibitishwa wa unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro, amesema "watoa huduma za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2022 waliripoti zaidi ya matukio 38,000 za unyanyasaji wa kingono na kijinsia katika Kivu Kaskazini pekee, ikiwa ni pamoja na viwango vya kutisha vya unyanyasaji wa kingono kwa watoto katika zaidi ya maeneo 1,000 ndani na karibu na kambi za watu waliohamishwa. 

Mwakilishi Maalum amesema kwamba wakati wa ziara yake DRC mwezi Juni alitishwa na shuhuda alizozisikia kutoka kwa wanawake na wasichana, ambao wengi wao walikuwa wamebakwa hivi majuzi na/au kubakwa na genge la watu na walikuwa wakiendelea kupokea matibabu. 

Huko Poland na Moldova, amesema, "Nilijionea mwenyewe mateso ya ajabu kwa wanawake, watoto na wazee, ikiwa ni pamoja na mazingira magumu yao kwa watu wasio waaminifu na mitandao ya wahalifu ambao kwao ufurushaji wa haraka na usio na kifani wa watu sio janga bali ni fursa ya biashara haramu na unyonyaji wa kingono.” 

Patten ameongeza Machi mwaka huu alitembelea tena Ukraine na "alikutana na walionusurika na kusikia maelezo yao ya kuhuzunisha mioyo ya unyanyasaji wa kikatili wa kijinsia unaoripotiwa kufanywa na askari wa Urusi." 

Amesema ripoti ya mwaka ya Katibu Mkuu "inaonesha wazi athari za kutokujali" na kuongeza kuwa "mpaka tutakapoongeza gharama na matokeo ya kutenda, kuamuru au kuunga mkono unyanyasaji wa kijinsia, hatutawahi kuzuia wimbi la ukiukaji kama huo." 

Nje ya Baraza hilo, Mwakilishi Maalumu wa Uingereza wa Kuzuia Ukatili wa Kijinsia, Tariq Ahmad, amesema, “tunapotupia jicho duniani kote, iwapo tunaitazama DRC, nilikotembelea Novemba, Ukraine, Myanmar, Sudan, na kwa hakika maeneo mengine mengi ya dunia, tunaendelea kuona matumizi ya unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro kama silaha halisi ya vita. Inatekelezwa kwa waathirika wengi wa vita, waathirika ambao wanatumaini kwamba wamenusurika mateso yao mabaya zaidi na kisha wanavunjwa katika njia yao ya chukizo kabisa.”