Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taka za kielektroniki ni jawabu la ajira iwapo zitasimamiwa vyema- ILO

Wafanyakazi katika kiwanda cha PT Toshiba Consumer Products Ind. wakiunganisha na kutengeneza bidhaa za kielektroniki kama televisheni huko Cikarang, Bekasi. Indonesia.
ILO/A. Mirza
Wafanyakazi katika kiwanda cha PT Toshiba Consumer Products Ind. wakiunganisha na kutengeneza bidhaa za kielektroniki kama televisheni huko Cikarang, Bekasi. Indonesia.

Taka za kielektroniki ni jawabu la ajira iwapo zitasimamiwa vyema- ILO

Tabianchi na mazingira

Shirika la kazi duniani, ILO limetaka hatua za haraka zichukuliwe ili kusimamia vyema taka za kielektroniki zinazozalishwa kote ulimwenguni ili  hatimaye ziwe chanzo cha ajira zenye utu.

Wito huo umetolewa katika mkutano wa ILO unaofanyika huko Geneva, Uswisi ambako wawakilishi wa serikali, wafanyakazi na waajiri wamesema wakati umefika kwa serikali kuwekeza zaidi kwenye mifumo ya kuchakata na kutumia upya taka za kielektroniki kwa kuzingatia kasi kubwa ya ongezeko la taka hizo ambazo kila mwaka huzalishwa tani milioni 50 zikiwa na thamani ya dola bilioni 62.

Ingawa hivyo ILO inasema ni asilimia 20 ya tani hizo za kielektroniki ndio hurejelezwa katika mazingira rasmi.

Kama hiyo  haitoshi, mazingira ambamo kwayo wafanyakazi wanaookota taka hizo ili ziweze kurejelezwa nayo ni magumu, wakiwa hawana mamlaka yoyote juu ya  ujira wa fedha zitokanazo na kazi hiyo ya suluba huku wakivunja taka hizo kwa mikono mitupu bila vifaa vya kujikinga.

Nikhil Seth ni mwenyekiti wa wa jopo la kimataifa la mashauriano kuhusu kazi zenye utu na taka ngumu anasema taka za kielektroniki zinazidi kuwa rasilimali muhimu kwa wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi kwenye mnyororo wa thamani kuanzia kwa wanaoziokota, wanaozitengeneza upya, wanaozitumia tena na wanaorejeleza vifaa vya umeme na vya kielektroniki, na wanaleta huduma bunifu na bidhaa kwenye soko na kurahisisha mzunguko wa uchumi.”

Hata hivyo Bwana Seth amesema lazima kuwa na mfumo bora zaidi wa kusimamia taka hizo kuliko hivi sasa ili

 Sauti ya Nikhil Seth

“Kuhakikisha kuwa taka za kielektroniki zinazozalishwa kwanza kabisa hazileti aina ya madhara ambayo taka za kielektroniki ambazo hazijachakatwa zinaweza kuleta kwa  mazingira, kwa afya ya binadamu na kwa wale wote wanaofanya kazi kwenye viwanda  ya usimamizi wa taka za kielektroniki.”


ILO imekumbusha pia umuhimu wa kutumia vijana ikisema kuwa vijana wana  ubunifu mkubwa wa kutumia taka za kielektroniki na hivyo ni fursa ya kuongeza nafasi za ajira.