Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upimaji VVUkwa wakati ni muhimili wa afya ya wafanyakazi- ILO

Dawa za kupunguza makali ya UKIMWI-ARV
Photo: Sean Kimmons/IRIN
Dawa za kupunguza makali ya UKIMWI-ARV

Upimaji VVUkwa wakati ni muhimili wa afya ya wafanyakazi- ILO

Afya

Katika takribani nchi 50 duniani imebainika kwamba maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi au VVU yanaongezeka na idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo bado iko juu. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya karibuni ya shirika la kazi duniani ILO iliyotolewa kuelekea siku ya ukimwi duniani itakayoadhimishwa kote duniani  tarehe Mosi disemba.

Ripoti hiyo inakadiria kwamba takribani watu 500,000 wenye umri wa kufanya kazi watafariki dunia ifikapo mwaka 2020 kutokana na magonjwa yanayohusiana na VVU.

Ripoti imeongeza kuwa na kibaya zaidi watu hawa watakuwa katika umri mdogo wa miaka ya 30 ambao kwa kawaida huwa ndio kilele cha uzalishaji wa maisha ya wafanyakazi

Kwa mujibu wa ILO hii sio tu hasara kwa maisha ya watu bali pia hasara katika biashara na uchumi kutokana na kwamba gharama ya vifo hivyo inaweza kuwa ni ya mabilioni ya dola na kutia dosari juhudi ya kusongesha mbele utimizaji wa ajenda ya maendeleo endelevu au SDGs.

Hata hivyo shirika hilo linasema hali hii inaweza kuepukwa kwa kuchukua hatua ya kwanza muhimu ambayo ni kupia kama isemavyo kauli mbiu ya siku ya Ukimwi duniani 2018,  “Ijue hali yako”  kauli ambayo ILO inasema ni kumbusho kwa kila mtu. Mkurugenzi mkuu wa ILO Guy Ryder amesema upimaji wa VVU katika maeneo ya kazi kunazaa matunda na kuokoa maisha na kuongeza kuwa kupitia mradi wa ILO wa ushauri nasaha na upimaji wa wafanyakazi kwa hiyari  kwa wafanyakazi(VCT@WORK)  wafanyakazi zaidi ya milioni 4 wamepimwa na wengine zaidi ya 100,000 walielekezwa kwenye kuanza kupata dawa za kupunguza makali ya ukimwi au ARVs.

Amesema hii inaonyesha bayana kwamba mahali pa kazi ni muhimu katika kupanua wigo wa huduma kwa wale ambao hawaipati ipasavyo.

Bwana Ryder amesema kitu kingine kinachotia moyo ni kwamba hivi sasa kuna machaguo mengi ya upimaji kwa mfano kuna vifaa vya mtu kujipima mwenyewe HIV ambavyo vinapatikana na ILO kwa kushirikiana na shirika la afya duniani WHO wamezindua sera ya upimaji binafsi wa VVU sehemu ya kazi.

Amesisitiza kuwa sera inayofanya kazi ya masuala ya VVU kazini inahakikisha kutokuwepo ubaguzi na kwa kushirikiana na wataalam wa afya katika maeneo husika ni muhimu endapo kama matunda mazuri ya upimaji yanatakiwa kuonekana.

ILO inasema kimataifa asilimia 25 ya watu wanaoishi na VVU hawajui hali zao, so inakusasa usiwe miongoni mwao kwa kuamua kuchukua hatua ya udhibiti wa afya yako. Pima ili usiachwe nyuma.