Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu huru wa UN alalamikia hukumu mpya dhidi ya Jaji Afiuni wa Venezuela.

Nyundo ya mahakamani
UNODC
Nyundo ya mahakamani

Mtaalamu huru wa UN alalamikia hukumu mpya dhidi ya Jaji Afiuni wa Venezuela.

Haki za binadamu

Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kupitia ripoti iliyochapishwa hii leo na baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, ameeleza kusikitishwa kwake na hukumu ya miaka mitano zaidi dhidi ya Jaji Maria Lourdes Afiuni wa Venezuela.

Mtaalamu huyo amesema hukumu hiyo ni kitendo kingine cha kumuadhibu na ni ukiukaji wa haki za binadamu.

Kundi la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wanaofuatilia uwekaji watu kizuizini koholela, lilitoa maoni yao mwaka 2010 likisema kuwa Jaji Afiuni Mora alikuwa amewekwa kizuizini kiholela.

Jaji Afiuni alikamatwa mwaka 2009 baada ya rais wa wakati huo Bwana Hugo Shavez kutaka jaji huyo afungwe kwa miaka 30 akimtuhumu kwa kumwachia huru mfanyabiashara Eligio Cedeño. Akiwa gerezani Bi Afiuni alinyanyaswa vibaya na mamlaka ilimnyima matibabu.

Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa majaji na wanasheria wa Umoja wa Mataifa Diego García-Sayán anasema, “Ni jambo la kusikitisha kwamba Jaji Afiuni anaendelea kushikiliwa kizuizini, na hukumu hii ya hivi karibuni ni wazi kwamba anaadhibiwa tena.”

Jaji Afiuni ambaye mara kadhaa hukumu dhidi yake imelalamikiwa na watalaamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, alishikiliwa gerezani kwa miezi 14. Mwaka 2011 kutokana na hali mbaya ya afya aliwekwa katika kizuizi cha ndani na miaka miwili baadaye alipewa msamaha lakini kwa masharti ya kutotoka nchini mwake na kutotumia mitandao ya kijamii.

Hukumu ya sasa imetolewa tarehe 21 mwezi Machi mwaka huu wa 2019 na mahakama mjini Caracas ambapo Bi Afiuni amehukumiwa miaka mitano jela kutokana na madai ya rushwa.

Mtaalamu amesema hukumu hii ya hivi karibuni inathibitisha wasiwasi wake mkubwa juu ya uhuru wa mahakama nchini Venezuela, upendeleo wa majaji na waendesha mashitaka na shinikizo wanalokabiliana nalo katika kushughulikia kesi za kisiasa.