Taasisi muhimu Venezuela hazifanyi kazi, hatma ya wananchi iko mikononi mwa mamlaka- Bachelet

5 Julai 2019

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema hali ya haki za binadamu nchini Venezuela imegubikwa na wingu zito akisema mustakabali wa taifa hilo uko mikononi mwa utayari wa mamlaka kuweka mbele maslahi ya wananchi wake.

Akiwasilisha ripoti ya uchunguzi wa haki za binadamu nchini humo mbele ya mkutano wa 41 wa Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, Bi. Bachelet amefafanua akisema kuwa taasisi muhimu na utawala wa sheria nchini Venezuela vimeporomoka kwa kiasi kikubwa huku uhuru wa kujieleza, kukusanyika na hata kushiriki shughuli za umma ni hatari na wahusika wanaweza kukumbwa na visasi.

Halikadhalika ametaja matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, mauaji ya mara kwa mara ya kiholela dhidi ya watu wengi akitaka yachunguzwe na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Ripoti hiyo pia imegusia kuporomoka kwa uchumi ambapo tangu mwaka 2013, pato la ndani la Venezuela limesinyaa kwa asilimia 44.3 ambapo Bi. Bachelet amesema,“Venezuela ni taifa lenye rasilimali zenye thamani, ikiwemo mafuta ya aina yake na akiba  ya dhahabu pamoja na vijana walio na mwamko, iko sehemu nzuri na mifumo yake kwa muda mrefu imetoa huduma za elimu na afya bure kwa watu wote. Janga la sasa linaathiri haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni pamoja na haki za kisiasa na kiraia.”

Kamishna huyo akahitimisha hotuba yake akisema,“kama nilivyosema huko Caracas, hatma  ya zaidi ya raia milioni 30 wa Venezuela, iko mikononi mwa utayari wa uongozi kuweka mbele haki za binadamu za wananchi badala ya matamanio yao ya kibinafsi, kiitikadi au kisiasa.”

Hata hivyo pamoja na changamoto zilizotajwa kwenye ripoti hiyo, Bi. Bachelet ameshukuru serikali ya Venezuela kwa jinsi ambavyo iliwawezesha kufika maeneo yote waliyotaka na pia kukubali kuendelea kuwepo nchini humo kwa maafisa wawili wa haki za binadamu ambao wataendelea kufuatilia na kutoa msaada wa kiufundi na ushauri kwa mamlaka.

Ripoti hiyo inafuatia uchunguzi ulioitishwa na Baraza hilo la  haki za binadamu kupitia azimio namba 39/1 ambapo wafanyakzi wa ofisi ya kamishna huyo walifanya ziara ya  uchunguzi huko Venezuela.

Halikadhalika walitembelea wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela waliosaka hifadhi Argentina, Brazil, Chile, Colombia, Ecuador, Mexico, Peru na Hispania huku Bi. Bachelet mwenyewe akitembelea Venezuela wiki mbili zilizopita.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter