Skip to main content

Misikiti na maeneo yote ya ibada yanapaswa kuwa kimbilio salama sio kumbusho la ukatili-Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza wakati wa ziara yake kwneye kituo cha utamaduni cha kiisalmu New York.
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza wakati wa ziara yake kwneye kituo cha utamaduni cha kiisalmu New York.

Misikiti na maeneo yote ya ibada yanapaswa kuwa kimbilio salama sio kumbusho la ukatili-Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ameungana na jamii ya Waislamu hapa New York Marekani kwa ajili ya kuonyesha mshikamano na waunini wote wa dini jiyo kutoka New York hadi New Zealand na zaidi.

Akizungumza na waumini waliokuwa wamekusanyika katika kituo cha utamaduni cha Kiislamu jijini New York, kwa ibada leo, bwana Guterres amesema ni wiki moja tangu mashambulizi ya kikatili katika misikiti miwili ya mji wa Christchurch nchini New Zealand ambapo amesema, “Mioyo yetu inasalia kuwa mizito na majonzi na huruma kwa familia za waathirika. Katika kipindi cha siku chache zilizopita, tumepata taarifa nyingi kuhusu waathirika na maisha yao. Tumesoma kuhusu watu kama Haji-Daoud, Husna, Naeem, Hussain na mashujaa wengine wanawake kwa wanaume ambao walipoteza maisha yao wakati wakijaribu kuokoa maisha ya wengine.”

Bwana Guterres amewataja pia wengine waliopoteza maisha yao akisema, “tumeangalia picha za mtoto Mucad wa umri wa miaka mitatu ambaye alipigwa risasi wakati akikimbilia alikokuwa mtekelezaji wa ukatili huo bila kuelewa hatari.Tumesikia pia maneno ya Farid, mwanamume ambaye amesikitishwa na kifo cha mkewe akitoa maneno ya msamaha, kwa sababu kama alivyosema, “hicho ndicho Islamu imenifundisha.”

Katibu Mkuu huyo amesema pia wameguswa na hatua ya uongozi kutoka kwa mamlaka lakini pia upendo na mshikamano wa watu wa New Zealand. 

Aidha mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema mashambulizi hayo yalikuwa ya kugadhabisha lakini sio ya kustaajabisha.

Bwana Guterres amesema kote duniani, kumekuwa na ongezeko la chuki dhidi ya waislamu na wayahudi na hotuba za chuki na chuki dhidi ya watu wenye misimamo tofauti huku akisisitiza hatari ya vitendo hivyo akisema, “hotuba za chuki zinaenea kama moto, mitandao ya kijamii inatumika kueneza chuki na tofauti za umma zinachochewa huku makundi ya kisiasa yanatangaza wazi kuhusu misimamo yao na uhusiano wao na Neo-Nazi au kurudia maneno au picha za kundi hilo.” Bwana Guterres ameongeza kwamba donda hilo linaenea na ni wajibu wa kila mtu kusaka tiba ikiwemo vyombo vya habari. 

Guterres akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa amesema ni muhimu kuhakikisha usalama katika maeneo ya ibada ambapo ametolea wito kamishna mkuu wa muungano wa usataarabu wa Umoja wa Mataifa, Miguel Moratinos kuweka mkakati wa hatua za Umoja huo kusaidia katika ulinzi wa maeneo ya ibada akisema, “natoa wito kwa muungano huo kuwasiliana na serikali na mashirika ya kidini kwa ajili ya usalama wa maeneo ya ibada, sababu ni dhahiri: misikiti na maeneo yote ya ibada na kutafakari yanapaswa kuwa kimbilio salama sio kumbusho la ukatili.”

Katibu Mkuu amesema leo na kila siku ni lazima kuchukua msimamo dhidi ya chuki dhidi ya waislamu na aina zote za chuki huku akielezea mshikmano wake na jamii akisema, “Niko hapa leo na moyo mzito na wenye majonzi kwa jamii hii na wanaohisi kama walengwa, hampo pekee yenu, dunia iko nanyi, Umoja wa Mataifa uko nanyi na mimi niko nanyi.”