Tunaishi zama za hatari sana- Adama Dieng

Adama Dieng, Mjumbe Maalum wa UN (Kati) kwenye mkutano wa pili wa kimataifa wa kundi la kimataifa la la kutetea haki ya dini, AIDLR
UN /Elma Okic
Adama Dieng, Mjumbe Maalum wa UN (Kati) kwenye mkutano wa pili wa kimataifa wa kundi la kimataifa la la kutetea haki ya dini, AIDLR

Tunaishi zama za hatari sana- Adama Dieng

Masuala ya UM

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari Adama Dieng ameonya hii leo dhidi ya zama za nyakati ngumu na za hatari za leo.

Bwana Dieng akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwenye   kongamano kwa ajili ya kukabiliana na hotuba za chuki ili kulinda vikundi vidogo vya kidini, wakimbizi na wahamiaji ametoa wito kukabiliana na kutovumiliana akitoa mfano wa mashambulizi ya hivi karibuni katika sehemu za ibada ikiwemo mauaji katika msikiti wa Christchurch New Zealand, mashambulizi ya makanisa Sri Lanka na mashambulizi ya hivi karibuni katika hekalu Marekani.

Mjumbe maalum huyo amesema, “kile ambacho kimefanyika hivi majuzi kimesababisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kusisitiza umuhimu wa kukabiliana na hotuba za chuki.”

Bwana Dieng ameongeza kuwa, wakimbizi na wahamiaji leo ni miongoni mwa walengwa, sababu tu ya utambulisho wao, akiongeza kuwa  “tunahitaji kuangalia vichocheo vya hali hii inayoshuhudiwa, ambayo kwa bahati mbaya inatukumbusha miaka ya 1930 wakati bara Ulaya, wayahudi waliochukuliwa kama wanayama na kulaumiwa kwa majanga mengi ikiwemo, mwelekeo wa kiuchumi wa wanyonge.”

Halikadhalika amesema dunia iko katika wakati muhimu katika vita dhidi ya chuki na misimamo mikali ambapo amesema, “hotuba za aina hii tunzozisikia leo hii katika miji mingi barani Ulaya ni hatari.”

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , António Guterres, hotuba za aina hiyo na mitizamo hasi dhidi ya wageni ni ishara kwamba dunia iko katika wakati muhimu kukabiliana na chuki na misimamo mikali wakati huu kukishuhudiwa mwamko wa makundi yanayounga mkono misimamo na uhusiano na manazi wa kisasa.

Ni katika muktadha huu ambapo kongamano hilo la dini, amani na usalma limefanyika likimulika wakimbizi na wahamiaji, kwani, “kwa sababu leo, kundi la watu hawa wanatishiwa, ameonya bwana Dieng.

Bwana Dieng amekumbusha kwamba hotuba za aina yoyote ambazo zinazua ubaguzi au chuki kwa misingi ya kidini zinapaswa kupingwa, “na kama alivyosema Katibu Mkuu, Antonio Guterres , tunahitaji kuhakikisha kwamba mitandao ya kijamii sio kivuli cha hatuba za aina hiyo.”