Mladenov alaani ukatili unaoelekezwa dhidi ya waandamanaji na vikosi vya Hamas Gaza

17 Machi 2019

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mchakato wa amani huko Mashariki  ya Kati Nickolay Mladenov amelaani vikali kampeni ya kamatakamata na ukatili unaotumiwa na vikosi vya Hamas dhidi ya waandamanaji ikiwemo wanawake na waoto huko Ukanda wa Gaza katika kipindi cha siku tatu zilizopita.

Bwana Mladenov kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema anasikitishwa na uhasama dhidi ya waandishi habari na wafanyakazi wa tume huru ya haki za binadamu ikiwemo kupigwa na nyumba zao kuvamiwa.

Mratibu huyo maalum amesema watu wa Gaza wanaokabiliwa na madhila ya muda mrefu walikuwa wanaandamana kupinga hali mbovu ya kiuchumi na kutaka hali ya maisha kuimarishwa katika ukanda huo.Aidha ameongeza kuwa ni haki yao kuandamana bila uoga na hofu ya kukandamizwa.

 

Halikadhalika bwana Mladenov ametoa wito kwa pande husika za Palestina kuanza mazungumzo na Misri kwa ajili ya kutekeleza makubaliano ya Cairo ya mwaka 2017 kikamilifu.

Pia ameelezea kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea na shughuli zake kuzuia ongezeko la machafuko, kuwaokoa watu wanaoteseka ukanda wa  Gaza, kuondoa vizuizi na kuunfa mkono juhudi za maridhiano.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii